1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yataka iendelee kuaminika Afghanistan

18 Desemba 2012

Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck anafanya ziara ya siku tatu nchini Afghanistan kwa lengo la kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani na kushadidia jukumu la Ujerumani nchini humo.

https://p.dw.com/p/174Qw
Rais Joachim Gauck akizungumza na wanajeshi wa Ujerumani katika kambi ya MarmalPicha: Reuters

Ziara yake hiyo ya kwanza iliyoanza jana, ameianzia Mazar-i Sharif kwenye makao makuu ya vikosi vya Ujerumani vinavyotumikia vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO -ISAF.

Akiwahutubia wanajeshi 2,000 kati ya 4,500 wa Ujerumani wanaotumikia vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuiaya ya kujihami ya NATO, Rais Gauck amewasifu wanajeshi, polisi na wasaidizi wa miradi ya maendeleo kwa moyo wao wa ujasiri na mchango wao katika kupigania amani na maendeleo.

Rais Gauck amesema "Kutokana na juhudi zetu za pamoja, tunabeba jukumu. Tumefikia makubaliano pamoja na washirika wetu wa Afghanistan na makubaliano hayo hatupaswi kuyakiuka. Tunataka kuendelea kuwa waaminifu na washirika wa kutegemewa. Inaniathiri sana ninapoona hakuna nchi yoyote nyengine inayosifiwa huku kama Ujerumani."

Gauck und Karzai in Kabul 18.12.2012
Rais Joachim Gauck akizungumza na rais Hamid Karzai mjini KabulPicha: picture-alliance/dpa

Gauck awashukuru wanajeshi wa Ujerumani

Katika ziara hii ya ghafla iliyojiri wiki moja kabla ya siku kuu za Krismasi, Rais Gauck aliyefuatana na mpenzi wake, Daniela Schadt, amedhamairia kutoa shukurani zake na kuonyesha mshikamano pamoja na wanajeshi, polisi na watumishi wa miradi ya maendeleo, wanaojikuta mbali kabisa na familia zao.

Rais wa Shirikisho ameshadidia umuhimu wa kuendelezwa mjadala nchini Ujerumani kuhusu hali namna ilivyo nchini Afghanistan, bila ya kutia chumvi.

Bundespräsident Gauck besucht Afghanistan
Rais Gauck na mpenzi wake Daniela Schadt na wanajeshi wa UjerumaniPicha: Reuters

Leo asubuhi Rais Gauck ameelekea mji mkuu Kabul ambako alipokelewa kwa heshima za kijeshi katika kasri la rais. Alikuwa na mazungumzo pamoja na rais wa Afghanistan, Hamid Karzai na kuzungumzia kuhusu ushirikiano katika sekta ya kiraia na maendeleo wakati vikosi vya kimataifa vitakapoondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka 2014.

Leo mchana Rais Gauck amepangiwa kukutana na wasomi wa dini ya kiislamu. Kutokana na hali mbaya ya hewa, Gauck alikawia kwa saa mbili kuwasili Kabul kutoka Mazari-Sharif.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir//dpa
Mhariri: Josephat Charo