Ujerumani yasikitishwa na mauaji ya Gaza
1 Machi 2024Kwenye ukurasa wake wa X, Baerbock aliandika siku ya Ijumaa (Machi 1) kuwa ameshtushwa akieleza kuwa watu walitaka misaada na kwa familia zao lakini baadhi wakafa.
Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, ambayo ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Israel, alisisitiza kuwa jeshi la Israel ni sharti lichunguze kikamilifu hofu kubwa na ufyatuliaji risasi uliotokea.
Soma zaidi: Watu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza
Wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas ilisema zaidi ya watu 100 waliokuwa kwenye foleni yakupokea misaada waliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel.
Lakini jeshi la Israel limekanusha madai hayo na kusema vifo hivyo vilitokana na mkanyagano.
Mataifa kadhaa yameilaani Israel kwa mkasa huo, zikiwemo India, China, Uturuki, Saudi Arabia, Misri na Jordan.
Wizara ya afya ya ukanda huo imesema idadi ya vifo tangu vita vilipoanza Oktoba 7, imepindukia 30,000.