Serikali ya Ujerumani yaridhia mpango wa pili wa wakimbizi
29 Januari 2016Makubaliano hayo yanatazamia kwamba wahamiaji ambao hawakukabiliani na mateso au ukandamizaji hawatoruhusiwa kuleta familia zao nchini Ujerumani kwa kipindi cha miaka miwili. Makamu wa Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameeleza hayo baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na gavana wa jimbo la Bavaria, Horst Seehofer.
Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema maneno hayo hayo wakati akizungumza na waandishi habari
“Pale tu makubaliano haya yatakapoanza kutekelezwa, wahamiaji walionahifadhi ya muda hawatoruhusiwa kuleta familia zao nchini Ujerumani,” alisema Kansela Angela Merkel.
Makubaliano hayo pia yanaazimia kuziorodhesha Morocco, Algeria na Tunisia kama nchi zilizo salama, na uamuzi huwo utarahisisha kuwarejesha makwao wahamiaji wanaotoka katika nchi hizo. Ujerumani ilifanya uamuzi wa aina hiyo mwaka jana kwa nchi kadhaa za Balkan ambazo raia wake walisemekana hawastahili kupewa hifadhi ya ukimbizi.
Hatua hizo zilizoafikiwa kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, zinatoa maelekezo ya kwamba kutakuwa na vituo maalum vitakavyochuja wahamiaji waliokuwa hawastahili kupewa hifadhi Ujerumani. Kwa muda mrefu vyama vya kihafidhina vya Merkel na Seehofer - CDU na CSU, vimekuwa vikichuana na chama cha siasa za mrengo wa shoto cha Social Democrats juu ya nani miongoni mwa waliopewa hifadhi anayefaa kunyimwa ruhusa na kuleta familia zao nchini.
Wajerumaji wamtaka Merkel ajiuzulu
Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya raia yaliyokusanywa na shirika la Insa kwajili ya gazeti la Focus umeonyesha kwamba asilimia 40 ya Wajerumani wanamtaka Kansela Angela Merkel kujiuzulu kutokana na sera yake ya wahamiaji, ambayo imeipelekea nchi hiyo kupokea zaidi wa wahamiaji milioni 1.1 wanaotafuta hifadhi mwaka jana.
Ujerumani ilisajili takriban watu milioni 1.1 kama wahamiaji wanaotafuta hifadhi mwaka jana, miongoni mwao takriban 430,000 ni Wasyria. Serikali ya Ujerumani inatarajia kupunguza idadi huyo kwa mwaka huu. Gabriel amesema asilimia 20 ya Wasyria ambao maombi yao ya kutafuta hifadhi bado yanashughulikiwa, kuna uwezekano wa kupewa hifadhi ya muda.
Makubaliano hayo bado yanahitaji kupitishwa na baraza la mawaziri pamoja na bunge la Ujerumani.
Maafisa wa Ujerumani kwa muda mrefu wamekuwa wakisisitizia umuhimu wa kuhakikisha kwamba wahamiaji walionyimwa hifadhi wanaondoka nchini. Na Merkel aliongeza kwamba serikali yake itafanya kazi na nchi tofauti wanapotokea wahamiaji wao ili suala hili lisonge mbele.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga