Ujerumani yarefusha muda wa jeshi lake nchini Mali
20 Mei 2022Matangazo
Wabunge 541 wa bunge la taifa, Bundestag, lenye zaidi ya viti 700 wamepiga kura kuunga mkono pendekezo la serikali ambalo litaongeza idadi ya wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali kutoka 1,100 na kufikia 1,400.
Kwa mara ya kwanza sehemu ya sheria hiyo inajumuisha kifungu kitachoruhusu wanajeshi wa Ujerumani kuondolewa nchini Mali iwapo hawatahakikishiwa usalama au upatikanaji wa huduma muhimu kutekeleza majukumu yao.
Uamuzi wa kurefusha muda na kuongeza idadi ya wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali umechangiwa kwa sehemu kubwa na hatua ya serikali ya Ufaransa ya kuondoa vikosi vyake kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya kuzuka msuguano na watawala wa kijeshi.