1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Watu zaidi ya 100,000 wafa kutokana na COVID-19

Zainab Aziz Mhariri:Jacob Safari
25 Novemba 2021

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa leo Alhamisi zinaonyesha Ujerumani imeingia hivi punde kwenye orodha ya nchi zilizokumbwa na vifo zaidi ya laki moja kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

https://p.dw.com/p/43T6p
Symbolbild 100.000 Covid-Tote in Deutschland
Picha: DW

Takwimu hiyo imethibitisha kuwa Ujerumani sasa imelemewa vibaya na mambukizi ya virusi vya corona. Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya Ujerumani Robert Koch ilisema imeorodhesha vifo vingine 351 katika muda wa saa 24 zilizopita na hivyo kufikisha jumla ya watu 100,119 waliokufa kutokana na COVID-19.

Katika bara Ulaya, Ujerumani ni nchi ya tano kuvuka alama hiyo, baada ya Urusi, Uingereza, Italia na Ufaransa. Tangu kuanza kwa mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona zaidi ya watu milioni 5.57 wamethibitishwa kuwa wameambukizwa. Kuongezeka kwa maambukizi ya corona kumeifanya serikali ya Ujerumani inayosubiriwa kushika hatamu kutangaza kuundwa kwa kundi jipya la wataalam wa afya watakaotoa ushauri jinsi ya kukabiliana na janga hili.

Kansela mteule wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela mteule wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: picture-alliance/AP/M. Sohn

Wakati idadi ya maambukizi ya kila siku ni kubwa kuliko ile ya msimu wa baridi kali uliopita kwa sasa idadi ya watu wanaokufa ni ndogo kulinganisha na msimu uliopita. Wataalamu wanasema hii ni kwa sababu ya chanjo,ambayo hupunguza athari kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo hospitali katika baadhi ya maeneo, hasa ya mashariki na kusini mwa Ujerumani, yanakabiliwa na shinikizo huku wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza wakitoa tahadhari kuwa watu wengi zaidi wanaweza kufa.

Meneja mkuu wa chama cha hospitali za mji wa Bavaria, Roland Engehausen, amesema jitihada zifanyike kupunguza kwa kasi idadi ya watu wanaoambukizwa vinginevyo tutakuwepo na hali ya kushangaza kati ya kipindi cha Krismasi na cha Mwaka Mpya. Kwa hali hiyo karantini na vizuizi vinanukia hasa kuelekea msimu wa Krismasi kwenye baadhi ya majimbo ya Ujerumani ambayo yamelemewa vibaya na maambukizi ya virusi vya corona.

Rais wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier amesema mzigo wa janga hili la corona ni mzito umma unatatizika kutafuta njia sahihi za kupambana na janga hili. Rais wa shirikisho, alikutana na familia za watu waliowapoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa wa COVID-19 mnamo mwezi Aprili. Wakati huo, idadi ya watu waliokufa ilikuwa zaidi ya watu 70,000. Wiki kadhaa baadaye, alitoa tamko wakati idadi hiyo ilipopanda hadi watu 80,000 nahadi leo wamekufa watu zaidi ya laki moja.

Watu zaidi waambukizwa virusi vya corona nchini Ujerumani
Watu zaidi waambukizwa virusi vya corona nchini UjerumaniPicha: Ricardo Castelan Cruz/Eyepix/abaca/picture alliance

Wakati huo huo Tume ya Ulaya leo Alhamisi imependekeza kwamba kuanzia Januari 10 mwaka ujao vyeti vya chanjo ya Covid-19 vya Umoja wa Ulaya viwe vinatumika kwa muda wa miez itisa baada ya mtu kupokea chanjo kamili, haliambayo inaashiria kufunguliwa njia ya kuongeza chanjom zan ziada kwenye pasi hizo.

Kwingineko wadhibiti wa madawa wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha matumizi ya  chanjo ya Pfizer-BioNTech ya COVID-19 kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano hatua ambayo Shirika la Afya Ulimwenguni WHO linahimiza kipaumbele kwanza kiwe ni kuwachanja watu wazima wote na watu walio katika mazingira magumu.

Vyanzo:/AP/DPA/RTRE/https://p.dw.com/p/43Mrd