Ujerumani yalipiga marufuku kundi la Hammerskins
19 Septemba 2023Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani iliyotolewa siku ya Jumanne (Septemba 19) ilieleza kuwa kundi hilo lenye takribani wafuasi 130 linalenga kueneza siasa kali za mrengo wa kulia na kibaguzi kwa kuzingatia itikadi ya Unazi Mamboleo.
Polisi walivamia nyumba 28 za wanachama wa kundi hilo kwenye majimbo kadhaa ya Ujerumani mapema siku ya Jumanne.
Soma: Kushamiri kwa itikali kali za kulia huenda kukazuwia uhamiaji wafanyakazi wenye ujuzi
Baadhi ya matawi ya kundi hilo na jengine liitwalo Crew 38, ambalo pia lina mafungamano na Hammerskins, pia yamepigwa marufuku.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, kundi hilo lililoanzishwa mwaka 1988 limekuwa na mchango mkubwa katika kuenezea itikadi kali za mrengo wa kulia barani Ulaya "ambazo ni kitisho kikubwa kwa demokrasia ya Ujerumani."