Ujerumani yajadili kuwarejesha wapiganaji wa IS kutoka Syria
18 Februari 2019Mwishoni mwa juma lililopita, Rais Donald Trump aliwataka washirika wake wa nchi za Ulaya, kuwarejesha nyumbani mamia ya wapiganaji wa kigeni wa kundi hilo la IS waliokamatwa na vikosi vya Kikurdi vya Syria vinavyoungwa mkono na Marekani.
"Marekani inazitaka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na nchi nyingine za Ulaya kuchukua zaidi ya wapiganaji 800 wa IS, ambao wamekamatwa na Marekani na wawafungulie mashtaka," Trump ameongeza kwamba, "vyenginevyo atalazimika kuwaachilia huru."
"Marekani haitaki kuwaona wapiganaji hao wakiingia barani Ulaya, ambako ndipo wanapotarajiwa kwenda," ameandika Trump katika ukurasa wake wa Twitter.
Tamko hilo la Marekani limezua mjadala nchini Ujerumani kuhusu kuwarejesha nyumbani raia waliojiunga na kundi hilo la kigaidi nchini Syria na Iraq.
Waziri wa mambo ya nje, Maas ana wasiwasi
Akimjibu Trump hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema sharti hilo la Trump litakuwa "vigumu sana kutekelezwa."
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD Maasa amesema kuwarejesha nyumbani watu hao na watoto wao pamoja na wake zao itawazekana iwapo watafunguliwa washtaka na kukamatwa pale tu wanapowasili nchini. Lakini Maas amesema kama hilo halitowezekana basi itakuwa vigumu kuwarejesha nyumbani.
Maas ameeleza kwamba kama mtu ana uraia wa Ujerumani basi ana haki ya kurudi Ujerumani. Lakini, kwavile Ujerumani ilikata uhusiano wa kidiplomasia na serikali ya Syria na hailitambui eneo la Kikurdi syria linalojitegemea, haitowezekana kuthibitisha utambulisho wa wafungwa hao.
Serikali za nchi za Ulaya zimekuwa na wasiwasi, kuhusu kuwarudisha nyumbani raia wao waliokwenda kuwaunga mkono IS kwa kupigana nchini Syria na Iraq. Wanahofia athari za kisiasa, zitakazotokana na kuwarejesha nyumbani watu makatili hasa kufuatia mfululizo wa mashambulizi yaliyofanywa na makundi ya kigaidi nchini Ufaransa, Ujerumani na kwengineko Ulaya.
Lakini maafisa wa Kikurdi nchini Syria wanasema hawana uwezo wa kubeba jukumu la kuwaweka kizuizini wapiganaji wageni wa kundi la IS. Wanadai kwamba kwa muda mrefu, wamekuwa wakizitaka nchi hizo kuwarejesha nyumbani raia wao.
Wamezionya nchi za Ulaya kwamba eneo lao halina utulivu, na kuna hatari ya wapiganaji hao wa IS waliokamatwa kutoroka kizuizini na kuingia katika nchi za Ulaya.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW
Mhariri: Caro Robi