1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaitaka Uturuki na Ugiriki kuacha chokochoko

1 Juni 2022

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema Kansela Olaf Scholz ameitolea mwito Uturuki kujizuia kuichokoza Ugiriki, wakati mvutano kati ya nchi hizo mbili ukiongezeka.

https://p.dw.com/p/4C9Dm
Türkei | Präsident Erdogan
Picha: Emin Sansar/AA/picture alliance

Msemaji wa ofisi ya Kansela wa Ujerumani ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Berlin kuwa, kutokana na hali ilivyo sasa Kansela  Scholz amesema ni muhimu kwa wanachama wote wa muungano wa jeshi la kujihami wa NATO akimaanisha Uturuki na Ugiriki, kusimama pamoja na kujizuia na chokochoko kati yao.

Msemaji huyo ameendelea kueleza, "Kuivamia anga ya Ugiriki na kurusha ndege juu ya visiwa vya Ugiriki sio sawa na hali hiyo inakwenda kinyume na mshikamano wa NATO." 

Soma pia: Uturuki yasisitiza kupinga Sweden na Finland kujiunga NATO

Msemaji huyo wa ofisi ya Kansela Scholz amesema Ujerumani imejitolea kusuluhisha mzozo kati ya Ugiriki na Uturuki kwa njia ya mazungumzo ya faragha na kwa misingi ya sheria za kimataifa.

Uturuki na Ugiriki, ambao wote ni wanachama wa NATO, kwa muda mrefu wamekuwa katika mzozo juu ya masuala mbalimbali ikiwemo mipaka ya baharini na anga, suala la wakimbizi pamoja na uhusiano na Cyprus iliyogawanyika kikabila.

Erdogan aishtumu Ugiriki kwa ukiukaji wa mipaka yake ya anga

USA | Ansprache Kyriakos Mitsotakis im Kongress
Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos MitsotakisPicha: Win McNamee/Getty Images

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema leo nchi hiyo inasitisha mazungumzo na Ugiriki, kutokana na mzozo na Waziri Mkuu wa Ugiriki kufuatia kile Ankara ilichokiita ukiukaji wa mipaka yake ya anga. Kauli ya Erdogan inaashiria kufufuka upya kwa mzozo kati ya mataifa hayo mawili.

"Nilimwambia waziri wangu wa mambo ya nje jana, na tumeisitisha mikutano yetu ya ngazi ya juu ya baraza la mikakati na Ugiriki."

Erdogan ameongeza kuwa, Uturuki imefuta pia jukwaa la ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, lililopewa jina la baraza la mikakati ya ngazi ya juu. Katika hotuba yake kwa wabunge wa chama tawala nchini Uturuki, Erdogan amesema anataka sera ya kigeni iliyo imara.

Soma pia: EU yaungana kuhusu Ukraine, lakini haitatoa uanachama wa haraka

Mwaka jana, baada ya kusimama kwa miaka mitano, nchi hizo mbili wanachama wa NATO zilianza tena mazungumzo ya kutatua tofauti zao juu ya bahari ya mediterania pamoja na masuala mengine. Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekuwa na mafanikio madogo huku nchi hizo zikiendelea kurushiana maneno.

Mvutano ulizuka upya wiki iliyopita baada ya Erdogan kusema Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis "hayupo tena" huku akimshtumu Waziri Mkuu huyo kwa kujaribu kuzuia mauzo ya ndege za kivita aina ya F-16 kwa Uturuki wakati alipokuwa ziarani nchini Marekani.

Jana Jumanne, Mitsotakis aliwaambia wanahabari baada ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kwamba, aliwaelezea viongozi wa Umoja huo juu ya uchokozi na uchochezi wa Uturuki ambao kamwe hauwezi kuvumiliwa na Ugiriki na pia Umoja wa Ulaya.