1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaipa Rwanda Euro mil. 56 kuboresha mazingira

2 Machi 2022

Rwanda na Ujerumani zimetia saini mkopo wa Euro milioni 56 kuisaidia Rwanda katika utekelezaji wa miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na utunzaji mazingira katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

https://p.dw.com/p/47s86
Ruanda Kigali Stadtansicht 2021
Picha: /AFP/Getty Images

Mkopo huo umetiwa saini mjini Kigali baina ya waziri wa uchumi wa Ujerumani Svenja Schulz anayefanya ziara ya siku 4 nchini Rwanda na mwenzie wa Rwanda Dr Uzziel Ndagijimana ambaye ni waziri wa fedha na mipango wa Rwanda.

Kabla ya kutia saini mkopo huo waziri huyo wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani na ujumbe anaouongoza walikutana kwa mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame katika Ikulu mjini Kigali.

Sehemu ya kwanza ni Euro milioni 30 zilizotolewa kama msaada wa serikali ya Ujerumani kwa serikali ya Rwanda na zitatumika katika miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kiasi kingine cha euro milioni 26 ni mkopo wenye riba nafuu kutoka benki ya maendeleo ya Ujerumani KfW.

UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow | Svenja Schulze
Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze.Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

'Tunahitaji ushirika na wanaojua wanakokwenda'

Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze amesema uamuzi wa Ujerumani wa kutoa kiasi hiki cha pesa ni ishara ya utayari wake katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa kwa kushirkiana na nchi ambazo zimeonyesha sera bora za kukabiliana na hali hiyo

"Nchi yenu imekuwa na ushirikiano na uhusiano mwema na Ujerumani kwa miaka zaidi ya 40 sasa na kwa hiyo ushirikiano katika kukabilina na mabadiliko ya hali ya hewa ni ushahidi kwamba sote tunakwenda pamoja katika juhudi za ulimwengu za kukabiliana na tatizo karne ya 21," alisema waziri Schulze.

Hata hivyo aliongeza kuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na utunzaji mazingira yanaweza kufanikiwa ikiwa tu yataweza pia kutambua changamoto za kijamii.

"Nahitaji kushirikiana zaidi na nchi ambazo ziko tayari na Rwanda ni miongoni mwa nchi ambazo zinajua kule zinakoelekea na kufanikiwa malengo yake,” alisema waziri huyo.

Feierlichkeiten zum Tag der Streitkräfte in Mosambik
Rais wa rwanda Pual Kagame.Picha: Estácio Valoi/DW

Waziri wa fedha na mipango wa Rwanda Dr Uzziel Ndagijimana ameipongeza serikali ya Ujerumani akitaja kwamba daima siku zote nchi mbili zimekuwa na ushirikiano mwema ambao umewezesha kufanikiwa katika miradi kadhaa ya ushirikiano.

"Makubaliano ya fedha hizi yamesainiwa baina yetu kwa ajili ya kusaidia mfuko maalum katika taasisi yetu ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, mathalan kusaidia miradi inayotunza mazingira nchini," alisema Ndagijimana.

Aliongeza kuwa kiasi kingine kitasaidia katika mradi mwingine unaoendelea wa kuufanya mji mkuu wa Kigali kuwa wa kijani. "Kwa hiyo nadhani huu ni msaada mkubwa ambao utasaidia kwenye mradi huu.”

Ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo

Baadaye waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani na ujumbe anaouongoza wakiwemo wajumbe kutoka kampuni ya Ujerumani ya BionTech, watengenezaji wa chanjo mbalimbali walitembelea eneo ambalo ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo za Covid-19 umeanza.

Waziri wa afya wa Rwanda Dr Daniel Ngamije alisema Rwanda imejizatiti kuanzisha kiwanda cha kutengeneza chanjo, kwa kuanzia na utengenezaji wa chanjo ya Covid-19 "ili kutatua tatizo tulilolitaja hapo kabla, kwa ushirikiano na BioNTech."

Deutschland | BioNtech | Biontainer
Rwanda pia imeanza ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo ya covid kwa kushirikiana na kampuni ya BionTech.Picha: Bernd Riegert/DW

"Kwa sasa tunaendelea kujenga uwezo kwa ajili ya kuwezesha uzalishaji wa chanjo hizo barani Afrika.Tunaendelea kujipanga na tunatazamia kuzipata chanjo za kwanza ndani ya kipindi cha miezi 24 kuanzia sasa,” alisema Dk. Ngamije.

Mapema Jumatano, waziri Schulze amekwenda eneo la kaskazini nje ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali kutembelea chuo cha mafunzo ya uchimbaji madini pamoja na machimbo ya madini aina ya Coltan kujionea teknolojia ya kisasa inayotumika.

Ujerumani imekuwa mshirika wa karibu wa Rwanda hasa kwenye sekta za uchumi na elimu na Ujerumani imesema mvuto huu wa kuendelea kushirikiana na Rwanda unatokana na sera ya Rwanda ya kujenga uchumi endelevu ambao unazingatia faida kwa wananchi wote kwa pamoja.