Ujerumani yaadhimisha miaka 35 kuangushwa Ukuta wa Berlin
9 Novemba 2024Madhimisho ya mwaka huu chini ya kaulimbiu ya "Kuuenzi uhuru" yatafunguliwa na Rais Frank-Walter Steinmeier kwenye eneo la kumbukumbu ya Ukuta wa Berlin. Eneo hilo lilianzishwa kutoa heshima kwa takribani watu 140 waliouawa wakijaribu kuikimbia iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Mashariki.
Ukuta wa Berlin uliangushwa mnamo Novemba 9 mwaka 1989 na siku hiyo inaadhimishwa nchini Ujerumani kama mwisho wa udikteta wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na kushindwa na itikadi ya kikomunisti ya Dola ya Kisovieti.
Baadaye leo jioni kutakuwa na onesho la burudani ya muziki na uwashaji wa taa kwenye lango mashuhuri la Brandeburg mjini Berlin, eneo ambako Ukuta wa Berlin ulikatisha na kuzitenganisha pande mbili za mji huo mkuu tangu mwaka 1961.