1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uhispania zitagaragazana katika Kombe la Dunia

2 Aprili 2022

Matayarisho ya Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 yalikumbwa na utata na manung'uniko ya siasa za kikanda na sasa droo iliyofanywa ya hatua ya makundi inazikutanisha nchi zenye uhasama mkubwa wa kisiasa

https://p.dw.com/p/49MpP
Katar Doha | FIFA Fußball WM 2022 Auslosung | Lothar Matthäus Deutschland Gruppe E
Picha: HAMAD I MOHAMMED/REUTERS

Ujerumani na Uhispania zitagaragazana katika Kombe la Dunia la mwaka huu baada ya droo ya hapo jana mjini Doha kuwapanga washindi hao wa zamani katika kundi moja. Ujerumani wamewekwa Kundi E pamoja na Uhispania na Japan wakisubiri mshindi wa mechi ya mchujo mwezi juni kati ya Costa Rica na New Zealand.

Mechi ya ufunguzi Novemba 21 itakuwa kati ya wenyeji Qatar na Equador ambao pia wamepangwa na Senegal na Uholanzi katika Kundi A. Cameroon imepangwa na washindi mara tano Brazil, Serbia na Uswisi katika Kundi G.

Tunisia iko Kundi D pamoja na mabingwa watetezi Ufaransa, Denmark na mshindi wa mechi ya mchujo kati ya Peru, Australia au Umoja wa Falme za Kiarabu. Ghana watakuwa na Uruguay, Korea Kusini na Ureno katika Kundi H.

Kundi F lina Morocco, Croatia, Ubelgiji na Canada. Kundi C lina Argentina, Saudi Arabia, Mexico na Poland. Mahasimu wa siasa za kikanda Marekani na Iran pia walipangwa katika kundi B pamoja na England, wakisubiri mshindi kati ya Wales, Scotland au Wales.

afp