1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na India zaashiria kutanua ushirikiano

5 Desemba 2022

Ujerumani na India zimeashiria kuwa tayari kutanua ushirikiano katika sera ya kiuchumi na mazingira, baada ya mkutano wa Jumatatu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/4KUnV
Indien Neu Delhi | Außenministerin Baerbock und Außenminister Subrahmanyam Jaishankar
Picha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Baada ya mkutano huo, katika ziara yake ya siku mbili nchini India, Baerbock amesema India haikuchukuwa tu uenyekiti wa kundi la mataifa 20 tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi la G20, lakini pia jukumu la ulimwengu mzima.

Alipoulizwa iwapo anaiona India kama taifa la kuchukuwa nafasi ya China katika uhusiano wa nchi hiyo na Ujerumani, Baerbock alikataa wazo hilo na kusema kuwa siku zote, India imekuwa mshirika wa Ujerumani na Umoja wa Ulaya.

Baerbock asema Ujerumani na India pia zimeshirikiana kimaadili

Baerbock ameendelea kusema kuwa kuhusiana na India, wameungana sio tu katika misingi ya ushirkiano wa kiuchumi lakini pia kupitia ushirikiano wa maadili, huku akiunga mkono sera za India zinazolenga kupunguza uzalishaji wa hewa chafu. Kuhusiana na sula hilo, Baerbock ameendelea kusema kuhusu utoaji wa hewa chafu kwa kila mtu, lazima waseme kwa uwazi kabisa kwamba India iko chini,  kabisa ya utoaji wa hewa chafu wa Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa kila mtu.

Jaishankar asema India itaendelea kununua mafuta ya Urusi

Russland Moskau | Präsident Wladimir Putin
Rais wa Urusi - Vladimir PutinPicha: Pavel Bednyakov/POOL/TASS/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, baada ya mkutano huo, waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar aliwaambia wanahabari kuwa India itatoa kipaumbele kwa mahitaji yake ya nishati na kuendelea kununua mafuta kutoka Urusi, wakati mataifa ya Magharibi yakianza kutekeleza azimio la ukomo wa bei kwa mafuta yake, ili kupunguza mapato yake yanayotumika kufadhili vita nchini Ukraine.

Jaishankar aliongeza kuwa sio sawa kwa mataifa ya Ulaya kutoa kipaumbele chao kwa mahitaji yao ya nishati lakini kuitaka India kufanya tofauti. Jaishankar pia amesema kwamba mataifa yatafanya maamuzi yake na kwamba ni haki yao. Jaishankar na Baerbock, pia wamezungumzia biashra mbali mbali katika ya mataifa hayo mawili, athari za ulimwengu za vita vya Urusi nchini Ukraine na ushirikiano katika mageuzi ya nsihati kutoka kwa mafuta ya viskuku.

Ujerumani na India zatia saini mkataba wa ushirikiano wa uhamiaji

Mataifa hiyo mawili pia yalitia saini mkataba wa ushirikiano wa uhamiaji na usafiri ambao utarahisisha watu kusoma, kufanya utafiti na kufanya kazi katika nchi hizo. Ujerumani ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa India barani Ulaya na zaidi ya Kampuni 1,700 za Ujerumani zinafanya kazi nchini India. Uwekezaji wa Ujerumani nchini India ni zaidi katika usafiri, vifaa vya umeme, ujenzi, biashara na magari.