1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na India zatiliana saini mkataba wa maendeleo

Josephat Charo
3 Mei 2022

Ujerumani na India zimetiliana saini mikataba ya ushirikiano inayolenga kuimarisha maendeleo endelevu. India itapokea msaada wa euro bilioni 10 kufikia 2030 kwa lengo la kuimarisha nishati safi isiyochafua mazingira.

https://p.dw.com/p/4AldP
Deutschland Narendra Modi zu Besuch bei Olaf Scholz
Picha: JOHN MACDOUGALL/AFP via Getty Images

Mikataba iliyosainiwa kati ya Ujerumani na India ilijumuisha masuala mbalimbali kuanzia msaada wa kiufundi hadi kuongeza matumizi ya nishati jadidifu na hydrojeni, hadi kupunguza gesi kutoka viwandani, kuwalinda viumbe hai na kuboresha matumizi ya ardhi ya kilimo. Shirika la mazingira la Ujerumai, Germanwatch, limeisifu mikataba hiyo likiieleza India kama taifa muhimu katika jitihada za ulimwengu kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Mkurugenzi wa shirika hilo anayeshughulikia masuala ya sera Christioph Bals, amesema kuharakisha mchakato wa kutafuta nishati mbadala India ni mchango muhimu kuhakikisha lengo la nyuzi 1.5 lililoanishwa katika mkataba wa Paris wa mwaka 2015 linafikiwa. Amezihimiza nchi nyingine tajiri zilizostawi kiviwanda za kundi la G7 zifikie makubaliano kama hayo na India.

Modi alisisitiza mwito wake kwa Urusi na Ukraine kukomesha mapigano akisema wanaamini hakuna upande wowote unaoweza kushinda katika vita hivyo. Scholz kwa upande wake aliikosoa Urusi kwa kuvunja sheria za kimataifa.

Lakini tofauti na Scholz, ambaye anaituhumu Urusi kwa kuziendea kinyume sheria za kimataifa, Modi alijizuia kutoa kauli yoyote ya kuikosoa Urusi. Urusi, ambayo ni msafirishaji mkubwa wa silaha kwa India, imewahi kuipongeza serikali ya waziri mkuu Modi kwa msimamo wake wa kutoegemea upande wowote katika mzozo huo.

Scholz ameialika India, Indonesia, Senegal na Afrika Kusini kuhudhuria mkutano ujao wa nchi za G7 utakaofanyika Ujerumani mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Maeneo mengine ya ushirikiano yaliyoafikiwa kati ya Ujerumani na India siku ya Jumatatu yanahusu uhamiaji, utafiti wa nyuklia na kuanzishwa kwa njia salama za mawasiliano kati ya serikali za nchi hizo mbili.

Scholz ameipongeza India kama mshirika mkubwa muhimu wa Ujerumani barani Asia na kusema ushirikiano wa karibu na India katika masuala ya kimataifa ni jambo alilotaka kuliendeleza na kulitanua.

Scholz amtaka Putin akomeshe vita Ukraine

Kansela Scholz alizungumzia mzozo wa Ukraine, akimtaka rais wa Urusi Vladimir Putin avifikishe mwisho vita, mauaji yasiyokuwa na maana na awaondoe wanajeshi wake kutoka Ukraine. Kansela huyo amesema yeye na waziri mkuu Modi walikubaliana mipaka haiwezi kubadilishwa kwa kutumia nguvu na machafuko. Modialisema amefurahi kwamba ziara yake ya kwanza nje ya nchi mwaka huu wa 2022 ilikuwa kwa rafiki yake kansela Scholz, akiitaja ziara hiyo kuwa ishara ya jinsi nchi zote mbili zilivyoupa kipaumbele uhusiano baina yao.

Deutschland Narendra Modi zu Besuch bei Olaf Scholz
Nerandra Modi, waziri mkuu wa India, kushoto, na Olaf Scholz, kansela wa Ujerumani mjini Berlin (02.05.2022)Picha: JOHN MACDOUGALL/AFP via Getty Images

Kiongozi huyo wa India pia alisema matukio yaliyoshuhudiwa hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya dunia yamedhihirisha jinsi amani na uthabiti unavyoweza kuyumbishwa kirahisi ulimwenguni, na jinsi nchi zilivyo na mafungamano na kutegemeana. Modi amesema mzozo wa Ukraine ulipoanza, India ilitoa wito mapigano yasitishwe na ikasisitiza umuhimu wa mdahalo kama njia ya pekee ya kuutanzua mgogoro huo. Modi aidha alisema wanaamini hakuna upande wowote utakaoshinda katikav ita hivi, kila mtu anateseka na ndio sababu wanaunga mkono amani.

Waandishi hawakuruhusiwa kuuliza maswali baada ya Modi na Scholz kuzungumza, kitu ambacho si cha kawaida kutokea katika afisi za kansela wa Ujerumani ambapo maswali angalau manne huruhusiwa wakati wa ziara za viongozi wa ngazi za juu. Afisa wa Ujerumani aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina, alisema uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na msisitizo uliotolewa na ujumbe wa India.

Kufuatia mkutano na Scholz, Modi ataitembelea Denmark kukutana na viongozi wa nchi za eneo la Nordic katika mkutano wa kilele kati ya nchi hizo na India. Baadaye atamtembelea rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

(afp, dpa)