1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Afrika Kusini zaujadili mzozo wa Ukraine

Sylvia Mwehozi
28 Juni 2023

Ujerumani na Afrika Kusini zinakusudia kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanya tofauti licha ya kuwa na misimamo inayotofautiana kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/4T8nJ
Annalena Baerbock alipozuru Afrika Kusini
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na mwenzake wa Afrika Kusini Naled PandorPicha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Waziri Annalena Baerbock, amefanya mazungumnzo na waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika Kusini Naledi Pandor na kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili walipokutana katika mji mkuu wa Pretoria. Ajenda zilizojitokeza ni pamoja na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya uchumi, utalii, mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na janga la Covid-19.

Suala la vita vya Urusi nchini Ukraine, pia lilitawala mazungumzo ya mawaziri hao wawili, huku waziri Baerbock akiitaka Urusi "kuacha kuishambulia" Ukraine katika mazungumzo yake na Pandor wakati wa ziara yake ya siku moja mjini Pretoria.Ujerumani na Afrika Kusini zaazimia kuimarisha ushirikiano wao licha ya kuwa na maoni tofauti katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Kuhusu tukio la uasi la mwishoni mwa juma lililofanywa na kundi la mamluki la Wagner, waziri Baerbock amewaeleza waandishi wa habari kwamba Ujerumani "haiingilii kati" kile alichokitaja kuwa "masuala ya Urusi", lakini akatahadharisha kwamba Ujerumani "inafuatilia kwa karibu" hali ya mambo ingawa msukumo wao unasalia kuwa vita vya Ukraine.

"Na hali ilivyokuwa mwishoni mwa juma lililopita inadhihirisha kwa mara nyingine tena kwamba Putin pia anahatarisha usalama wa nchi yake kwa vita hivi ambavyo ni kinyume na sheria za kimataifa, na ndiyo maana wito wetu wa dharura ni kwamba vita hivi lazima viishe. Hilo liko mikononi mwa Rais wa Urusi. Sote duniani tunatamani amani. Na ndio maana amani ndio jambo muhimu zaidi kwetu," alisema waziri Baerbock.

Annalena Baerbock na Cyril Ramaphosa
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akisalimiana na Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: South African Presidency

Kwa upande wake Waziri Pandor amesema kwamba "Afrika Kusini na Ujerumani zina misingi mingi inayofanana katika masuala ya amani na usalama, haki za binadamu, mabadiliko ya tabia nchi, na maendeleo endelevu ya kiuchumi". Kuhusu jaribio la uasi la mwishoni mwa juma waziri Pandor, anasema "halitaathiri dhamira yetu ya kuendelea kushirikiana na nchi zote mbili, kama ilivyokubaliwa na marais ambao ni sehemu ya ujumbe wa amani wa  Afrika. Tayari tumechukua hatua kutokana na mialiko iliyotolewa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ya kuitaka Afrika Kusini kushiriki katika mjadala kuhusu mpango wa amani ambao umewasilishwa na Ukraine.”

Ujerumani imeikosoa Afrika Kusini kwa kushindwa kulaani kwa uwazi uvamizi wa Urusi huku nchi hiyo ikijinasibu kutoegemea upande wowote katika mzozo huo. Msimamo wa Afrika Kusini kuhusu vita vya Ukraine, umekuwa ukifuatiliwa kwa uangalifu tangu balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini Reuben Brigety alipotoa madai kwamba Afrika Kusini ilipakia kwa siri silaha katika meli ya Urusi iliyokuwa imetia nanga kwenye kambi ya wanamaji karibu na Cape Town mnamo mwezi Desemba.Waziri Baerbock aitaka Afrika Kusini kuamua kuhusu Ukraine

Nchi hiyo pia inakabiliwa na kitisho cha mvutano mwingine wa kidiplomasia mnamo mwezi Agosti pale itakapokuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa muungano wa nchi zinazoibukia kiuchumi za BRICS ambao unaundwa na Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, baada ya kumwalika Rais Vladimir Putin kuhudhuria mkutano huo licha ya waranti ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Vyanzo: dpa/ap/Reuters