Ujerumani leo inakumbuka miaka 20 tangu kuanguka Ukuta wa Berlin
9 Novemba 2009Maadhimisho rasmi ya kumbukumbu ya miaka 20 ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin yameanza katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin. Maelfu ya watu wamemiminika katika mji huo kuhudhuria kumbukumbu hiyo inayoadhimishwa leo Jumatatu. Watu hao wamemiminika katika uwanja wa Postdam ambako kuna alama ya ukuta wa bandia wa Berlin. Ukuta huo wa bandia utaangushwa ikiwa ni kuashiria hatua ya kuangushwa kwa ukuta wa zamani uliokuwa ukizitenganisha Ujerumani Magharibi na Mashariki, mnamo Novemba 9, mwaka 1989.
Wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa yote ya Umoja wa Ulaya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Rais wa Urusi, Dmitri Medvedev wamealikwa kuungana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika sherehe hizo.
Katika ujumbe wake alioutoa jana Jumapili kupitia televisheni, Kansela Merkel alisema Novemba 9 ni siku ya furaha katika historia ya sasa ya Ujerumani. Aidha, Bibi Merkel alipongeza kazi iliyofanywa na wanaharakati wa vyama vya kiraia na Kanisa katika kuanzisha mapinduzi ya amani yaliyopelekea kumalizika kwa sera za kikomunisti za Ujerumani ya Mashariki.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton amesifia kitendo cha kuanguka kwa Ukuta wa Berlin akisema kitendo hicho ni moja ya matukio muhimu katika karne ya 20. Hayo ameyaeleza katika ziara yake ya kwanza mjini Berlin tangu ashike wadhifa huo.
Bibi Clinton amesema tukio hilo la Novemba 9 mwaka 1989 lilibadilisha sura ya kisiasa katika bara lote. Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema Ujerumani hadi leo inawashukuru wananchi wa Marekani kwa hatua yao ya kuiunga mkono Ujerumani miaka 20 iliyopita.