Ujerumani kuwarejesha wanawake wa IS kutoka Syria
23 Novemba 2019
Itakuwa ni mara ya kwanza kwa Ujerumani kuwarejesha watuhumiwa wa aina hiyo.
Maafisa nchini Ujerumani wameamuru mwanamke Mjerumani, anayeaminika kuwa ni mwanachama wa kundi linalojiita "Dola la Kiislamu" IS , kurejeshwa nchini mwake kutoka katika kambi nchini Syria, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Ijumaa.
Gazeti la Spiegel limemtambua mwanamke huyo kuwa ni Laura H. mwenye umri wa miaka 30 kutoka katikati mwa Ujerumani, likisema kuwa aliondoka nchini na kujiunga na wanamgambo wa jihadi mwaka 2016. Yeye pamoja na watoto wake watatu wanaripotiwa kuishi hivi sasa katika kambi inayoendeshwa na Wakurdi ya al-Hol kaskazini mwa Syria. Wanatarajiwa kuwasili nchini Ujerumani , 'katika siku za karibuni' kwa kusafiri kupitia mji wa Wakurdi wa Erbil nchini Iraq, kwa mujibu wa gazeti la Siegel.
Siku ya Ijumaa, maafisa wa Ujerumani walithibitisha kuwa watoto watatu "Wajerumani wanaoshikiliwa kaskazini mwa Syria, wataweza kuondoka kwenda Iraq pamoja na mama yao." Hata hivyo , hawakuthibitisha jina la mama yao ama kutoa taarifa zaidi.
Wanawake walioko kizuwizini
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, maafisa wa Ujerumani wamekuwa wakimchunguza mama huyo kwa shaka ya kuwa mwanachama wa shirika la kigaidi na kuwatelekeza watoto.
Washukiwa wanawake wa kundi hilo la "Dola la Kiislamu", tayari wamekuwa kizuwizini na kufikishwa mahakamani nchini Ujerumani, lakini mashitaka yamekuwa tu katika hatua ya washukiwa ambao wamesafiri kurejea nyumbani kwa matakwa yao ama wamerejeshwa na nchi nyingine. Iwapo suala la laura H. litathibitishwa , litakuwa ni mara ya kwanza kwa Mjerumani kurejeshwa nchini.
Duru za usalama nchini Ujerumani zinaamini kuwa zaidi ya wanachama 80 wa IS ambao ni Wajerumani wanaendelea kushikiliwa nchini Syria. Serikali mjini Berlin ilitangaza hivi karibuni kuwa itatoa maamuzi ya kurejeshwa kwa wanawake waliolewa na wanamgambo wa Jihadi kwa misingi ya kesi kwa kesi.
Watoto kadhaa tayari wamekwisha rejeshwa kutoka katika kambi katika mashariki ya kati. Mapema mwezi huu, mahakama nchini Ujerumani iliamuru kuwa akina mama mbali mbali wanaohusishwa na IS pamoja na watoto wanalazimika kurejeshwa pamoja , kwasababu watoto hao walikuwa wanategemea "ulinzi na malezi ya mama zao."