Ujerumani: Kura ya imani kuitishwa Desemba 16
13 Novemba 2024Kura hiyo ya imani itafungua njia ya kwenda kwenye uchaguzi wa mapema mnamo mwezi Februari.
Kansela Scholz amesema hayo katika tamko la serikali, alilolitoa bungeni mapema Jumatano, wiki moja baada ya serikali yake ya mseto kuvunjika.
Katika tamko hilo Kansela Scholz pia alizungumzia juu ya uhusiano na Marekani na juu ya vita vya Ukraine.
Scholz amesema uhusiano na Marekani ni muhimu, hata baada ya kuchaguliwa Donald Trump. Ameeleza kwamba uhusiano huo ndiyo umekuwa msingi wa mafanikio ya Ujerumani kwa miaka mingi.
Juu ya vita vya Ukraine Kansela Scholz amesema Ujerumani inapaswa kuendelea kuisaidia nchi hiyo inayojihami dhidi ya Urusi.
Kulingana na Scholz, hakuna maamuzi yatakayopitishwa nchini Ujerumani yatakayoipuuza Ukraine.
Hata hivyo ametamka wazi kwamba msaada huo hautatolewa kwa gharama za mafao ya uzeeni au kwa gharama za huduma za matunzo. Scholz pia amesema atawania muhula wa pili ingawa chama chake cha SPD bado hakijaamua juu ya mgombea wake.