1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kumchagua rais wake kupitia baraza maalum

13 Februari 2022

Ujerumani siku ya Jumapili itamchagua rais wake kuiongoza nchi hiyo. Rais wa sasa wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier anatazamiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

https://p.dw.com/p/46wS7
Deutschland | Bundespräsident Frank-Walter Steinmeier
Picha: Britta Pedersen/dpa-Zentralbild/picture alliance

Steinmeier amejinyakulia sifa kama mtetezi asiyechoka wa maadili ya kidemokrasia, wakati ambapo kuibuka tena kwa siasa kali za mrengo wa kulia na janga la virusi vya corona imekuwa changamoto kubwa kwake.

Wagombea wengine watatu wanaowania nafasi ya urais ni pamoja na Gerhard Trabert daktari na mgombea binafsi aliyependekezwa na chama cha mrengo wa kushoto, Die Linke, Max Otte, mwanauchumi aliyeteuliwa na chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD, ambacho kinafuata siasa kali za mrengo wa kulia, ingawa yeye mwenyewe ni mwanachama wa CDU.

Mwingine ni Stefanie Gebauer, mwanafizikia mwenye umri wa miaka 41, kutoka chama cha siasa za wastani wa mrengo wa kulia Free Voters au Freie Waehler kama kinavyojulikana kwa Kijerumani.

Anaungwa mkono na vyama vya serikali ya muungano

Steinmeier anaungwa mkono na vyama vyote vilivyoko kwenye serikali ya muungano ya sasa, kikiwemo chama chake mwenyewe cha Social Democratic, SPD, chama cha Kijani kinachotetea ulinzi wa mazingira na chama cha kiliberali FDP.

Hata hivyo anaungwa mkono pia na muungano wa vyama vya kihafidhina CDU/CSU. Kwa kuungwa mkono na vyama hivyo, Steinmeier, mwenye umri wa miaka 66 anatarajiwa kushinda kwa urahisi katika uchaguzi huo.

Rais wa Ujerumani anachaguliwa kila baada ya miaka mitano kupitia baraza maalum linalotokana na wabunge 736 pamoja na wawakilishi 736 kutoka majimbo yote 16, na hivyo kuifanya idadi jumla ya wajumbe watakaomchagua rais kuwa 1,472

Berlin | Frank-Walter Steinmeier wird Bundespräsident
Frank-Walter Steinmeier akipongwezwa kwa maua baada ya kushinda uchaguzi wa Februari 12, 2017Picha: AXEL SCHMIDT/AFP/Getty Images

Miongoni mwa wajumbe hao ni baadhi ya watu mashuhuri, akiwemo kiungo wa kati wa timu ya Bayern Munich anayeichezea pia timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani, Leon Goretzka, aliyeteuliwa na chama cha SPD.

Uchaguzi wa urais ambao kwa kawaida hufanyika katika jengo la Bunge la Ujerumani, utafanyika katika jengo la Paul Loebe linalopakana na ofisi ya kansela katikati ya Berlin, ili kuendana na vigezo vilivyowekwa kutokana na janga la virusi vya corona kwa watu kukaa umbali wa mita kadhaa.

Steinmeier aliyehudumua mara mbili kama waziri wa mambo ya nje katika serikali ya Angela Merkel, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais wa Ujerumani mwaka 2017, akichukua nafasi ya Joachim Gauck.

Mwanasiasa maarufu anayetegemewa Ujerumani

Steinmeier mwenye Shahada ya Udaktari wa Sheria, amekuwa mmoja wa wanasiasa maarufu na wanaotegemewa sana nchini Ujerumani. Amerudia kuonya kuhusu kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo nchini Ujerumani. Aidha, ametoa wito wa kusimama pamoja katika kukabiliana na janga la COVID-19.

Wadhifa wa urais nchini Ujerumani ni wa kiishara tu, na iwapo atachaguliwa tena, Steinmeier atakuwa rais wa nchi, huku Kansela Olaf Scholz akiendelea kuwa mkuu wa serikali ya Ujerumani.

Marais wa Ujerumani wanaweza kugombea nafasi hiyo kwa muda usiozidi mihula miwili, ingawa Steinmeier, ambaye anatarajiwa kuchaguliwa tena, atakuwa mtu wa nne pekee kufanya hivyo.

(AFP, DW https://bit.ly/3JmE8ZD)