Ujerumani: Hatma ya wakimbizi milioni 1.8 haijulikani
18 Julai 2019Idara kuu ya uandikishaji wa wahamiaji imethibitisha kwamba watu hao milioni 1.8 wenye nasaba za uhamiaji waliomba ulinzi wa kisheria mwaka uliopita nchini Ujerumani. Hali hiyo inatokana na watu hao kutokuwa na uhakika iwapo wataruhusiwa kuishi nchini.
Watu walioomba ulinzi wa kisheria ni wahamiaji kutoka Syria, Irak na Afghansitan na idadi yao imeongezeka kwa asilimia 6 na kufikia milonioni 1 .8. mnamo mwaka uliopita. Idara kuu ya takwimu ya Ujerumani imesema watu wengine wapatao 101,600 walioongezeka katika idadi ya wale wanaoomba kupewa uhakika wa vibali vya kuwaruhusu nchini Ujerumani.
Idadi kubwa ya watu hao ni wale waliokuja Ujerumani kwa mara ya kwanza, miaka mitano iliyopita. Asilimia 62 ya wahamiaji hao wanatoka Syria, Irak na Afghanistan:kutoka Syria ni watu 529,000, kutoka Irak 138,000 na wengine 131,000 wanatoka Afghanistan. Idadi kubwa ya watu hao wamepewa vibali vya muda vya kuwawezesha kukaa Ujerumani.
Miongoni mwa wahamiaji hao, 129,000 ni wale ambao maombi yao yamekataliwa. Hilo ni ongezeka la watu 15,000 kulinganisha na mwaka 2017. Watu hao wamo katika hati hati ya kufukuzwa nchini lakini serikali ya Ujerumani imechelewesha hatua ya kuwaondoa nchini.
Wakati huo huo uchunguzi uliofanyika umebainisha kwamba nusu ya wajerumani hawana moyo wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Uchunguzi huo umebainisha kwamba chuki dhidi ya wahamiaji imeongezeka licha ya ukweli kwamba sasa ni idadi ndogo tu ya wahamijai wanaokuja Ujerumani.
Waliofanya uchunguzi huo wamesema kuwa sera ya kizalendo ya mrengo wa kulia imekuwa jambo la kawaida miongoni mwa wazawa. Watafiti hao kutoka wakfu wa Friedrich Ebert wamesema wanasiasa wa mrengo wa kati wamepoteza dira ya demokrasia. Wakfu huo ulitokea ripoti ya uchunguzi uliofanywa tangu mwaka 2002.
Na kwa mujibu wa uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na wataalamu kutoka chuo kikuu cha Bielefeld katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Ujerumani, umeonyesha kwamba asilimia 54.1 ya wajerumani walioulizwa nchini Ujerumani kote sasa wana mtazamo hasi juu ya wakimbizi wanaoomba kibali cha kuishi nchini Ujerumani.
Chanzo:https://p.dw.com/p/3MFTb