Ujasusi wa Marekani waendelea kuitesa Ujerumani
23 Julai 2013Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linamnukuu mwenyekiti wa wabunge wa chama cha Kijani, Christian Stöbele, asiyetaka kusikia hoja kwamba mkuu wa Shirika la Ujasusi la Ujerumani, Gerhard Schindler, anapaswa kujiuzulu, ati kwa kuwa tu Shirika la Usalama la Marekani lilikuwa likifanya udokozi kwenye mawasiliano ya balozi za Ujerumani mjini Brussels, New York na Washington.
“Siamini kwamba tunapaswa kumtoa kafara Schindler, maana si kweli kwamba alivumilia matendo hayo.“ Anasema Stöbele.
Lakini mhariri anaona la kumkingia kifua Schindler linapaswa kufanywa na wataalamu wa masuala ya usalama, na sio wanasiasa akina Stoebele, maana ujasusi na siasa vina mizizi tafauti.
Ndoto za 'Muungano Mkubwa' zafifia?
Mhariri wa gazeti la Rheinische Post anazungumzia uchaguzi ujao hapo Septemba 2013, ambapo wengine wanasema kutalazimika kuwepo kwa serikali ya muungano utakaovijumuisha vyama vya CDU/CSU na kile cha upinzani cha SPD. Lakini uwezekano huo umekuwa ukipingwa vikali na SPD
Mwenyekiti wa wabunge wa chama cha SPD katika jimbo la North-Rhine Westphalia, Norbert Romans, ameshasema wazi kwamba hakubaliani na uwezekano huo wa ushirika na muungano wa CDU/CSU wa Kansela Angela Merkel.
“Sisi tunapambana, na nina hakika kuwa Peter Steinbrück ndiye Kansela ajaye. Hatuhitaji muungano na Wekundu, Weusi wala Kijani,” amesema Romans.
Lakini mhariri anamuonya mwanasiasa huyo kwamba hisabati ya siasa, haichelei wala kuchelewa kubadilika, naye asinunue mbeleko mwana akiwa bado hajazaliwa.
Kubakwa akabakwa, kufungwa akafungwa
Gazeti la Neue Osnabrücker linageukia siasa, au tuseme mikasa, ya kimataifa huko kwenye Ghuba ya Arabuni, ambako mwanamke mmoja, raia wa Norway, alichomwa msumari mmoto juu ya donda bichi. Ilikuwaje?
Mwanamke huyo aliyekuwa akiishi Dubai alidai kubakwa, na akaenda polisi kuandikisha malalamiko. Lakini jaji akamuhukumu yeye kifungo cha miezi 16 jela, kwa kosa la kufanya mapenzi nje ya ndoa.
Mhariri anaiita hiyo kuwa ni hukumu ya msituni – ya mnyonge kunyongwa na haki yake akanyimwa. Mwanamme anayetuhumiwa kubaka yuko huru, kana kwamba alichokitenda lilikuwa kosa dogo tu la kupuuziwa.
Sasa mwanamke huyo amepewa msamaha na ufalme wa Imarat, baada ya malalamiko kutoka sehemu mbalimbali duniani. Na mhariri anahitimisha kwa kusema, kumbe nyuma ya majumba makubwa ya Dubai, bado kuna mfumo wa kikale wa kisheria!
Kweli Hizbullah magaidi lakini....
Mhariri wa gazeti la Neue Westfälische, ambaye anazungumzia uamuzi wa Umoja wa Ulaya kuliweka kundi la Hizbullah la Lebanon kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.
Mhariri huyo anasema Umoja wa Ulaya haupaswi kupinda vigezo vyake vya haki, demokrasia, na sheria. Ilikuwa lazima kuiweka Hizbullah mahala pake, maana kweli ni magaidi.
Lakini ikiwa hatua hiyo itakuwa na athari kwa uhai na ufanyaji kazi wa Hizbullah, hilo ni suala jengine. Maana, hakuna uwezekano wa siku za karibuni kulitenganisha kundi hilo na siasa za ndani ya Lebanon na eneo zima la Mashariki ya Kati, hasa kwa vile, tangu awali halikuwahi kuutegemea Umoja wa Ulaya wala Marekani kwenye kufanya shughuli zake.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Kölner Stadt-Anzeiger, Neue Osnabrücker, Neue Westfälische
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman