Uingereza yaidhinisha mradi tata wa kuchimba mafuta na gesi
27 Septemba 2023Kampuni kubwa ya Equinor iliyobobea kwenye sekta ya uchimbaji nishati za visukuku ndiyo imepewa kandarasi hiyo na inatarajiwa kuwekeza kiasi dola bilioni 3.8 kuendeleza eneo hilo liitwalo Rosebank lenye hifadhi ya mafuta na gesi asili.
Tangazo la utoaji kibali hicho yumkini litafufua upya mjadala juu ya mkakati wa Uingereza wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kiasi wiki moja tangu serikali ya waziri mkuu Rishi Sunak kuondoa uwezekano wa nchi hiyo kufikia malengo ya kuachana na nishati chafuzi ifikapo mwaka 2050.
Wanaharakati wa mazingira wanaupinga mradi wa Rosebank wakisema unakwenda kinyume na dhamira ya Uingereza ya kuyapa kisogo matumizi ya nishati zinazichafua mazingira.
Hata hivyo serikali ya nchi hiyo imesema mradi huo ni muhimu katika kuiwezesha Uingereza kujitegemea kwa nishati.