1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiRwanda

Uingereza na Rwanda zatia saini mkataba mpya

5 Desemba 2023

Uingereza na Rwanda leo zimetia saini mkataba mpya katika juhudi za kufufua mpango tata wa serikali ya Uingereza wa kuwahamishia Rwanda waomba hifadhi na wahamiaji wengine

https://p.dw.com/p/4ZoZN
Wahamiaji wawasili katika visiwa vya Kanari chini Uhispania mnamo Oktoba 21,2023
Wahamiaji wawasili katika visiwa vya Kanari chini UhispaniaPicha: IMAGO/ABACAPRESS

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly, amekutana na mwenzake wa Rwanda Vincent Biruta mjini Kigani kutia saini makubaliano hayo na kuokoa azma hiyo ya Uingereza baada ya mahakama ya juu ya nchi hiyo mwezi uliopita kupinga mipango ya awali iliyoitaja kuwa kinyume cha sheria. Cleverly amesema anaamini mkataba huo mpya na Rwanda utashughulikia masuala yote yalioibuliwa na mahakama ya juu wakati ilipopinga mipango ya serikali ya nchi hiyo ya kuwapeleka waomba hifadhi hao nchini Rwanda.

Mahakama ya Uingereza ilisema kuwa ni hatari kwa wahamiaji kupelekwa Rwanda

Mahakama ya juu ya Uingereza ilitoa uamuzi dhidi ya mpango huo wa Rwanda na kutoa sababu kuwa kulikuwa na hatari kwamba wakimbizi waliohamishiwa nchini humo wangekabiliwa na hali ngumu ya kutathimniwa madai yao ama kurudishwa katika nchi yao ya asili kukabiliwa na mateso.

Soma pia:Uingereza kusaini na Rwanda mkataba mpya wa kuwahamisha wahamiaji

Wakati wa mkutano na wanahabari mjini Kigali, Cleverly ameongeza kuwa wameshirikiana kwa karibu na washirika wao wa Rwanda kuhakikisha kwamba masuala hayo yanashughulikiwa. Hata hivyo, Cleverly amesema Uingereza haijatoa ufadhili wowote kwa Rwanda unaohusishwa na kusainiwa kwa mkataba mpya kuhusu uhamiaji haramu. Waziri huyo wa Uingereza ameongeza kuwa Rwanda haijaomba pesa hizo na kwamba mpangilio wa kifedha ambao bila shaka ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa, unaonesha gharama itakazopata Rwanda kupitia mabadiliko ambayo ushirikiano huo umesababisha katika mifumo yake ya kisheria na kitaasisi.

Cleverly amesema kushughulika na uhamiaji ni muhimu na sio chaguo linalokosa malipo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly katika mkutano wa pamoja wa wanahabari na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken mjini London mnamo Juni 20, 2023
Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly Picha: Leon Neal/AP/picture alliance

Uamuzi wa mahakama ya juu wa mwezi uliopita ulikuwa pigo kwa waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ambaye yuko chini ya shinikizo kali kupunguza uhamiaji nchini humo ambao sasa umefikia rekodi ya watu 745,000 mwaka jana huku wengi wakiwasili nchini humo kupitia njia halali. Hapo jana serikali ya Uingereza, ilitafuta kupunguza idadi ya wahamiaji wanaowasili nchini humo.

Soma pia:Waziri Mkuu wa Uingereza Sunak kuendelea na mpango wa Rwanda licha ya hukumu ya mahakama

Sunak ameapa kudumisha mpango huo unaokabiliwa na utata kwa kuingia katika mkataba huo mpya.

Majibu ya Sunak pia yanajumuisha kupitishwa kwa sheria ya dharura bungeni kuiorodhesha Rwanda kama taifa salama na kutamatisha mzunguko wa changamoto za kisheria.

Sheria inayoitangaza Rwanda kuwa taifa salama unatarajiwa kuchapishwa wiki hii

Mkataba huo mpya unatarajiwa kufuatiwa baadaye wiki hii na kuchapishwa kwa sheria inayoitangaza Rwanda kuwa taifa salama, iliyotungwa kuzuia changamoto za kisheria dhidi ya ndege zilizopangwa za kuwahamisha waomba hifadhi.

Chini ya mpango huo uliokubaliwa mwaka jana, Uingereza inakusudia kuwapeleka nchini Rwanda maelfu ya waomba hifadhi waliofika kwenye fukwe zake bila ruhusu ili kuzuia wahamiaji kuvuka eneo la ujia wa bahari wa Uingereza kuingia nchini humo kutoka Ulaya kwa kutumia boti ndogo.

Kwa upande wake, Rwanda imepokea malipo ya awali ya dola milioni 180 milioni kwa ahadi ya pesa zaidi

kufadhili malazi na utunzaji wa watu wowote waliohamishiwa nchini humo.