1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuwapeleka takribani waomba hifadhi 6,000 Rwanda

Hawa Bihoga
30 Aprili 2024

Waziri wa Afya Uingereza Victoria Atkins, amesema serikali ya nchi hiyo ina mpango wa kuwapeleka nchini Rwanda wahamiaji wapatao 6,000 kwa mwaka huu, baada ya kuchapisha maelezo mapya kuhusu mpango huo wenye utata.

https://p.dw.com/p/4fLQK
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak.Picha: Toby Melville/AP Photo/picture alliance

Waziri huyo aliyasema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Sky News na kuongeza kuwa wahamiaji zaidi ya 2,000 kati ya hao wanaweza kusakwa na kuwekwa kizuizini kabla ya kusafirishwa.

Soma zaidi: Bunge la Uingereza lapitisha sheria tata ya wahamiaji kupelekwa Rwanda

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo imesema kwamba wahamiaji waliowasili nchini Uingereza baina ya Januari 2022 na Juni 2023 wanaweza kukataliwa maombi yao ya hifadhi na kupelekwa nchini Rwanda.

Kulingana na takwimu rasmi, zaidi ya watu 57,000 waliwasili kwa boti ndogo baada ya kujaribu kuvuka bahari na kuingia nchini humo katika kipindi cha miezi 18.