Uingereza kujitoa kutoka Umoja Ulaya bila makubaliano
30 Machi 2019Uamuzi wa kuukataa mpango uliofupishwa kidogo wa makubaliano ya talaka kati ya May na Umoja wa Ulaya imeliacha suala la kujitoa kutoka Umoja huo katika hali ya sintofahamu kwa sasa, lini na ama hata iwapo Uingereza itajitoa kutoka Umoja wa ulaya, na kulitumbukiza suala hilo la mzozo wa Brexit lililodumu kwa muda wa miaka mitatu sasa katika kiwango kikubwa cha kutoeleweka linaelekea wapi.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anapaswa kujiuzulu mara moja baada ya kufanya majadiliano ya muda ya kurefusha uanachama wa muda wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya , gazeti la kila siku la Telegraph limesema katika toleo lake la leo Jumamosi.
"Hapaswi kuona , ama kupaswa kuambiwa , kwamba wakati anaweza kukutana na Umoja wa Ulaya kujadili kurefushwa kwa Brexit, ni kitu cha kawaida kwamba ndio amefika mwisho wa barabara. Ni lazima ajiondoe, kwa ajili ya Brexit, kwa chama chake na demokrasia yenyewe," gazeti hilo liliandika katika uhariri wake.
Gazeti la Telegraph limekuwa kimsingi kama gazeti linalopendelewa na wanachama wa chama cha May cha Conservative.
Hata hivyo uwezekano wa kuwa na waziri mkuu mpya kuongoza awamu ijayo ya majadiliano ya Brexit ilikuwa haitoshi kuweza kuwavutia wabunge jana Ijumaa, baadhi yao wakihofia makubaliano yake yanaiacha Uingereza ikifungwa katika Umoja wa Ulaya iwapo mazungumzo ya hapo baadaye ya biashara yatavunjika.
Changamoto kutolewa madarakani
May, ambaye amenusurika changamoto ya kumtoa madarakani mwezi Desemba , amedokeza bungeni jana kwamba angehitaji kuitisha uchaguzi mkuu wa taifa kuweza kupata wingi kwa ajili ya kupitisha sheria ya Brexit.
"Uwezekano wa bibi May , kuazisha uchaguzi na kuongoza kundi la wabunge wa chama chake cha Conservative kupata wabunge wengi watakaofikia theluthi ya wabunge wote bungeni , ni ya kichekesho," gazeti la Telegraph imewaambia wasomaji wake.
Gazeti lenye wasomaji wengi nchini Uingereza la The Sun , limemtaka May kujiuzulu katika taarifa yake ya ukurasa wa mbele katika toleo lake la Jumatatu.
Gazeti la daily Mail , gazeti jingine ambalo linaunga mkono Brexit limeueleza uamuzi wa bunge kupiga kura dhidi ya mipango ya may kuwa ni "usaliti kwa Brexit" katika ukurasa wake wa mbele.
Katika muda wa dakika chache baada ya bunge kupiga kura , hatua iliyotokea wakati maelfu ya waungaji mkono Brexit wakifanya maandamano nje ya bunge , rais wa halmashauri ya Umoja wa ulaya Donald Tusk alisema viongozi wa Umoja wa Ulaya watakutana Aprili 10 kujadili kuondoka kwa Uingereza kutoka kundi hilo la mataifa.
Viongozi kadhaa wa Ulaya wamesema kuna nafasi halisi kwamba Uingereza sasa itajiondoa bila kupata makubaliano, hali ambayo makampuni yanahofia itasababisha mtafaruku kwa uchumi huo wa tano mkubwa duniani.
Insert: Ripoti Kitojo
Mhariri: Iddi