1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Ujerumani na Israel ni wa kustaajabisha

12 Mei 2015

Ni vigumu kufikiri kuwa Ujerumani na Israel zinaweza kudumisha uhusiano wa kawaida baada ya mauaji ya halaiki ya wayahudi ya Holocaust. Ni kawaida na wakati huo huo si kawaida.

https://p.dw.com/p/1FOSZ
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Israel na serikali ya Ujerumani zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia miaka hamsini iliyopita, chini ya miaka ishirini baada ya kukamilika kwa vita vya pili vikuu vya dunia na chini ya miaka ishirini baada ya majeshi ya muungano wa soveit kuwashinda wanazi waliongozwa na Adolf Hitler.

Chini ya miaka ishirini baada ya kukamilika kwa mauaji ya halaiki ya wayahudi ambayo yalisababisha mauaji ya wayahudi milioni sita barani Ulaya yaliyofanyika katika kambi za mateso zilizoanzishwa hususan kuwaangamiza wayahudi kwa kiwango kikubwa cha kustajaabisha.

Kuaminiana licha ya yaliyopita

Mateso ya ya kila namna yakiwemo kuondolewa kwa lazima, kutengwa kufungiwa katika kambi za mateso, kunyanyaswa na kuuawa kwa kutumia sumu ilikuwa ni ukiukaji wa kinyama wa ustaarabu.

Waandamanaji wakibeba bendera za Ujerumani na Israel
Waandamanaji wakibeba bendera za Ujerumani na IsraelPicha: AP

Licha ya kuwa makubaliano ya kulipa fidia kati ya Israel na Ujerumani ya magharibi yalitiwa saini mwaka 1952, ilikuwa bado si jambo la kuingia akilini kwamba wajerumani na waisrael wangeweza kuanzisha na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia.

Umma uliokuwa na ghadhabu ulifanya maandamano Israel kupinga kuanzishwa kwa uhusiano huo wa kidplomasia jambo ambalo linaeleweka katika hali ya kibinadamu na kisiasa ikizingatiwa historia ilivyokuwa.

Uhusiano wa Israel na Ujerumani ni muujiza

Miaka hamsini baadaye, Ujerumani na Israel zimedumisha uhusiano wa karibu, suala linaloonekana kama miujiza ya kisiasa. Maelfu ya vijana wa Israel wanazuru Ujerumani kwa likizo au hata kuja kuishi Ujerumani.

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na Rais wa Israel Reuven Rivlin
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na Rais wa Israel Reuven RivlinPicha: Getty Images/C. Koall

Kiasi ya waisrael laki mbili wana uraia wa nchi hizi mbili Israel na Ujerumani. Ujerumani taifa lililofanya mauaji ya halaiki ya wayahudi ya Holocaust ndilo taifa maarufu nchini Israel mbali na Marekani.

Kwa upande mwingine, kufanya kazi Kibbutzim kulipendelewa na wajerumani katika miaka ya sitini na sabini. Hivi sasa raia wa Ujerumani wanazuru Israel kuuona mji mtakatifu.

La muhimu zaidi serikali za Ujerumani na Israel zinashirikiana kwa karibu na kuaminiana. Ujerumani ndilo taifa barani Ulaya ambalo Israel inaweza kuiamini na kuitegemea zaidi.

Licha ya mizozo kuhusu sera za Israel za kuedendelea na makaazi ya walowezi wa kiyahudi au msimamo wa Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu dhidi ya kuwepo taifa huru la Palestina, usalama wa Israel unasalia kupewa kipaumbele na serikali ya Ujerumani kama alivyotangaza Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mbele ya bunge la Israel la Knesset mwaka 2008 bila ya kuwepo pingamizi Ujerumani.

Ujerumani mara nyingi huwa nchi pekee ya umoja wa Ulaya inayosimama na Israel kila wakati jambo ambalo ni la kusikitisha kwa nchi inayozingirwa na maadui. Ni jambo lisilo la kawaida kuwa Ujerumani ni mshirika wa karibu zaidi wa Ujerumani hii leo. Ni uhusiano ambao hakuna angeliyedhani ungewezekana miaka hamsini iliyopita.

Ukawaida wa uhusiano hauaminiki lakini ukawaida huo unajikita katika yasiyo ya kawaida. Machungu na makovu ya zamani bado yanakumbukwa vyema na nchi zote mbili. Kuuawa kwa wayahudi barani ulaya na wanazi ni sehemu ya chimbuko la nchi hizo mbili na mtazamo wa kila mmoja kwa mwingine. Ndilo jambo linalotambulisha tabia za mataifa hayo mawili.

Kuna wanayotofautiana pia

Mambo ya kushangaza kuzihusu nchi hizo mbili pia hujitokeza katika matukio ya kila siku ya kijamii na kisiasa. Waisrael wanawaweka wajerumani katika hadhi ya juu lakini wajerumani hawawezi kusema hivyo kuwahusu waisrael hasa kwasababu ya mzozo wa mashariki ya kati.

Makumbusho ya wahanga wa mauaji ya haliki ya Holocaust
Makumbusho ya wahanga wa mauaji ya haliki ya HolocaustPicha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Cha kustaajabisha, idadi kubwa ya wajerumani wanawahurumia wapalestina ambao wanajiona kama waathiriwa wa madhila ya waisrael na hapo ndipo uhusiano kati ya Israel na Ujerumani unapoanza kuwa tete.

Lakini mbali na hayo, huku wayahudi wakiondoka Ufaransa kwasababu hawahisi kuwa salama huko, hakuna wayahudi wanaondoka Ujerumani kwenda Israel kutokana na hofu ya chuki dhidi yao. Badala yake ukweli wa mambo ni kuwa wayahudi wanahamia Ujerumani. Idadi ya wayahudi imeongezeka mara mbili nchini Ujerumani katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Huo ndiyo muujiza wa pili. Wayahudi wanataka kuishi tena Ujerumani. Hata hivyo linalotia doa hilo ni kuwa polisi wanahitajika kushika doria katika vituo vya kuwatunza watoto, masinagogi na makaburi ya wayahudi kuihakikishia jamii ya wayahudi usalama wao.

Hiyo ndiyo sura mbovu ya chuki dhidi ya wayahudi ambayo bado ipo mpaka sasa. Lakini miaka sabini baada ya mauaji ya mamilioni ya wayahudi, uhusiano kati ya wajerumani na waisrael ni mzuri wa kiajabu.

Mwandishi: Alexender Kurdascheff

Msimulizi: Caro Robi

Mhariri:Josephat Charo