Uhuru wa kiraia, haki za binaadamu mashakani Tanzania - LHRC
4 Julai 2018LHRC ilichapisha ripoti yake siku ya Jumatano (Julai 4) kuhusiana na uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika na kuzibainisha sheria zinazokwaza uhuru huo, huku kikifungua mjadala unaotaka wananchi kujitokeza na kuanza kuzijadili sheria hizo.
Kituo hicho, ambacho kila mara kimekuwa kikifanya tathmini kuhusu hali ya haki za binadamu na uhuru wa kiraia, kilisema baadhi ya sheria zilizoanza kutumika katika miezi ta karibuni zinawabinya raia kutetea uhuru wao.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kuzindua ripoti yake hiyo, LHRC ilisema sehemu kubwa ya wa sheria hizo, zikiwamo zile zilizopigiwa kelele wakati wa upitishwaji wake, "zinakinzana na misingi iliyoanishwa katika katiba ya nchi na nyingine zikionekana kuwa kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia."
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa kituo hicho, Anna Henga, mashirika ya kutetea haki za binadamu sasa yameanza kukaribisha mjadala wa kitaifa unaolenga kuzianisha sheria hizo ambazo utekelezaji wake umeshuhudia baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii "ikimulikwa mara mbili."
"Kuwepo kwa sheria kama ile ya Kupambana na Uhalifu Mitandaoni ya 2015 katika wakati ambapo kunashuhudiwa ongezeko kubwa la mitandao ya kijamii kumewasukuma wanaharakati wa mitandao ya kijamii kwenda mahakamani kuhofia kuwa kuwepo kwake kutawasababishia wananchi wengi kutumbukia matatani," alisema mkurugenzi huyo.
Mapema mwezi uliopita serikali ilianza kuitekeleza rasmi sheria inayowahusu watoa maudhui katika mitandao ya kijamii hatua ambayo ilishuhudia mitandao mingi zikiwamo blogi, redio na televisheni za mtandaoni kusitisha huduma zake kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vilivyomo kwenye sheria hiyo inayowataka kujisajili rasmi kwenye Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA).
Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef