1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUlaya

Uhispania yaongeza nguvu uokoaji janga la mafuriko

4 Novemba 2024

Uhispania imewapeleka maelfu ya wanajeshi wa nyongeza kwenda upande wa mashariki mwa nchi hiyo ulioathiriwa na mafuriko makubwa baada ya kusuasua kwa juhudi za uokoaji na msaada kwa walioathirika.

https://p.dw.com/p/4maqJ
Janga | Kikosi cha jeshi kikiwa katika uokoaji Uhispania
Kikosi cha jeshi kikiwa katika uokoaji UhispaniaPicha: Susana Vera/REUTERS

Jeshi la nchi hiyo tayari liliwatuma askari 5,000 mnamo mwishoni mwa juma kusaidia kusambaza maji na chakula, kusafisha mitaa pamoja na kuzuia uhalifu.

Mapema hii leo Waziri wa Ulinzi wa Uhispani Margarita Robles alikiambia kituo cha redio cha taifa kwamba wanajeshi wengine 2,500 wanatumwa kuongeza nguvu. 

Soma pia:Vifo vilivyotokana na mafuriko ya Uhispania vyapanda hadi 200

Idadi ya watu waliokufa kutokana na janga hilo la mafuriko yaliyolikumba jimbo la Valencia na wilaya jirani ya Paiporta imepanda na kufikia 217 huku juhudi za kuwatafuta wengine wasiojulikana walipo zikiendelea. 

Hapo jana umma wenye hasira uliwarushia tope Mfalme Felipe na mkewe Malkia Letizia wa Uhispania walipokwenda kutoa pole kwenye wilaya ya Paiporta.