Uhamishaji raia Aleppo waendelea
19 Desemba 2016Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura juu ya azimio la kuwapeleka waangalizi mjini Aleppo ili kuangalia usalama wa raia.
Zaidi ya raia 1000 wamefanikiwa kuondolewa kutoka katika eneo la mwisho linaloshikiliwa na waasi katika mji wa Aleppo Syria mapema leo baada ya masaa kadhaa ya ucheleweshwaji.
Daktari Ahmad Dbis ambaye anaongoza timu ya madkatari na wafanyakazi wa kujitolea wanaoratibu zoezi hilo, amesema idadi hiyo ya raia inayojumuisha wanawake na watoto wamewasili katika eneo la magharibi la mji huo.
Wakati huo huo Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, limesema watu wanaokadiriwa kufikia 500 pia wameondoka kutoka vijiji viwili kaskazini magharibi vilivyokuwa chini ya mzingiro wa waasi.
Zoezi la kuwahamisha raia lilisimamishwa ijumaa baada ya makubaliano kukwama na vikosi vya upande wa serikali vimesisitiza uwepo wa mabadilishano kabla ya kumruhusu mtu yeyote zaidi kuondoka chini ya makubaliano ambayo Urusi na Uturuki wameyaratibu.
Mabasi yachomwa moto
Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria limesema jumla ya mabasi sita yaliyokuwepo katika msafara wa kuelekea Foua yameharibiwa kwa kuchomwa moto na kundi la Fath al-Sham Front lenye mafungamano na Al-Qaeda.
Dereva mmoja wa basi ameuawa katika shambulio hilo la jana ambalo lilisababisha zoezi hilo kukwama kwa muda kabla ya kuendelea leo asubuhi. Kiasi ya raia 5500 na wapiganaji 3000 tayari walikwisha ondolewa chini ya makubaliano kabla ya kuvunjika na raia wengi pamoja na waasi waliosalia wamesema kwamba wanahofia kuteswa au kuuawa ikiwa wataangukia mikononi mwa mikono ya serikali.
Kupelekwa waangalizi
Huku hayo yakiarifiwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura leo juu ya azimio lililowasilishwa na Ufaransa juu ya kuwapeleka haraka waangalizi wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Aleppo nchini Syria, hatua ambayo Ufaransa inasema ni muhimu katika kuzuia "mauaji makubwa" yanayofanywa na vikosi vya Syria na hususan wanamgambo walioziteka ngome za waasi.
Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa Samantha Power amelezea rasimu ya azimio hilo kuwa "mswaada huo umejumuisha mambo yote ya kiusalama na uokoaji ulio wa heshima na kwa ajili ya kupata misaada ya kibinadamu kwa wale wanaoamua kubaki mashariki mwa Aleppo na msisitizo juu ya ulinzi ambao umekosekana Syria katika kipindi chote cha mgogoro huu."
Mswaada wa azimio hilo unautaka Umoja wa Mataifa na taasisi nyinginezo kufuatilia zoezi la kuwahamisha raia na kumtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kushauriana na pande zote kwa haraka ili kuwaruhusu waangalizi.
Ufaransa na Urusi , ambazo ziliwasilisha rasimu ya maazimio yanayokinzana, zilifikia maelewano baada ya masaa matatu ya mazungumzo ya ndani kwa mashauriano na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/AP/AFp
Mhariri: Daniel Gakuba