1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhalifu na vijana barani Afrika

21 Februari 2019

Hadithi kuhusu uchunguzi katika michezo ya redio ya DW zinazungumzia changamoto zinazowakabili vijana barani Afrika.

https://p.dw.com/p/2lAyK
LbE Crime Fighters Produktion Kenia 2019
Picha: DW/A. Gensbittel

Awamu ya tatu ya michezo ya Karandinga inaangazia zaidi wanafunzi wanaopambana na walimu wanaotaka kufanya nao mapenzi, ili wawape maksi nzuri, wagonjwa vijana wanaokumbana na waganga waongo, na vijana ambao wanafatilia kwa ukaribu kile kilichoko nyuma ya habari zinazowazunguka.

Katika utamaduni wa vipindi vya Noa Bongo Jenga Maisha Yako, mfululizo wa michezo ya redio ya DW yenye mafanikio, hadithi za Karandinga zinatoa mawazo muhimu na kuwapatia wasikilizaji elimu wanayoweza kuitumia katika maisha yao ya kila siku.

 

Crime Fighters Teil 3 Many Facts one Truth

Taarifa Nyingi, Moja ya Kweli

Sherehe za kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha vijana zinagubikwa na mauaji ya kikatili ya Musa Bamafor. Mkandarasi wa ujenzi huo alipigwa vibaya hali iliyosababisha kifo chake kutokana na majeraha makubwa. Jammo na Kayla, wenye umri wa miaka 17 kwa bahati walisikia purukushani hiyo, lakini hawakufanikiwa kuwaona wahusika ni kina nani.

Wanataka kufahamu zaidi, hivyo wanaanzisha uchunguzi wao binafsi kwa kushirikiana na rafiki yao Fidelis. Je Bamafor alikuwa kweli fisadi, kama kila mtu anavyosema, na hiyo inaweza kuhusishwa na kifo chake? Wapelelezi vijana wanaofanya kazi hiyo bila malipo, wanapata taarifa za kushangaza, ambazo zinabainisha kuwa sio kila taarifa inayoenezwa inaweza kuaminika. Wanagundua njama katika mtandao ambao taarifa za uwongo zimechangia pakubwa. Hadithi hii imeandikwa na Pinado Abdu Waba (Nigeria).

 

Crime Fighters Teil 3 Secret of the Bones

Siri ya Mifupa

Wakati Zuri, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja anatekwa usiku wa manane kwenye mtaa wa mabanda, wazazi wake wanahuzunika. Nani atakuwa amemtaka mtoto wao wa kiume na kwa nini? Watoto kadhaa katika eneo hilo ambao awali walipotea katika mazingira ya kutatanisha, hawakupatikana tena. Polisi wanaanza haraka kumtafuta Zuri.

Aina fulani ya ushahidi unamnyooshea kidole Lindia, mganga wa kienyeji, lakini anadai kwamba hana hatia. Baba yake Zuri anamuomba mganga mwingine wa kienyeji, Shava, amsaidie kumtafuta mtoto wake. Shava anajulikana katika jamii hiyo na inasemekana ana nguvu sana. Mganga yupi kati ya hao wawili ni mkweli na anaweza kuaminiwa? Na je, juhudi za kumpata Zuri akiwa hai zitafanikiwa? Hadithi hii imeandikwa na Sonwabiso Ngcowa (Afrika Kusini).

 

DW Crime Fighters Teil 3 School of Graft

Ufisadi Shuleni

Mwalimu mkuu wa shule ya Jomvu, Bibi Gongo, anaanguka mbele ya walimu wenzake, wazazi na wanafunzi wakati wa hafla maalum ya Siku ya Wazazi na anapoteza fahamu. Polisi hatimaye wanagundua kuwa aliwekewa sumu-lakini kwa nini? Je ni kwa sababu ya walimu wenzake wenye wivu waliokitaka cheo chake? Au mtu ambaye hakukubaliana naye kuhusu kampeni yake ya kupinga rushwa kwenye shule hiyo?

Inspekta Upide anapeleleza, lakini anapata mafanikio kidogo. Awa, mwalimu kijana aliyeko katika mafunzo shuleni hapo, anaanza kutafuta vidokezo yeye mwenyewe. Kidogo kidogo, anagundua kwamba kilichotokea kwa Bibi Gongo huenda kinatokana na mpango wake wa siri katika shule hiyo-kufichua dhulma za unyanyasaji wa kimapenzi dhidi ya wanafunzi unaofanywa na walimu ambao wanawaahidi kuwapa maksi nzuri. Hadithi hii imeandikwa na James Muhando (Kenya).