Ugomvi wa Colombia na wanamgambo wa FARC umekwisha
16 Agosti 2017
"Tunashuhudia tukio la kihistoria... ningebidi kusema, pumzi za mwisho. Kamishna wa masuala ya amani Sergio Jaramillo ameiita hivyo hivyo, pumzi za mwisho za mzozo uliodumu miaka 53. Tunapaoiona kontena ya mwisho ikitoweka, tunaamini kweli hii ni awamu ya mwisho ya kuachilia mbali silaha."Amesema hayo rais wa Colombia, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2016, Juan Manuel Santos, katika hotuba yake iliyotangazwa moja kwa moja na televisheni toka eneo la kaskazini la Pondores, kaskazini mwa Colombia.
Vikosi vya jeshi la wanamapinduzi wa Colombia kwa ufupi FARC, vuguvugu la wapiganaji wa chini kwa chini lililoundwa mwaka 1964 kufuatia uasi wa wakaazi wa mashambani, wametia saini maakubaliano ya amani mwezi wa Novemba na watageuka kuwa chama cha kisiasa mkutano mkuu utakapotishwa kuanzia Agosti 27 hadi septemba mosi inaayokuja mjini Bogota, mji mkuu wa Colombia."Zoezi la kuhakiki mpango wa kuweka chini silaha na kusalimisha silaha limekamilika na wakati huu, linaanza pia chini ya usimamizi wa Umoja wa mataifa zoezi la kujiunga FARC na maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya nchi yetu". Amesema kwa upande wake Ivan Maruquez, mmojawapo wa viongozi wa FARC , mwakilishi wa zamani wa vuguvugu hilo katika mazungumzo ya amani yaliyodumu miaka minne nchini Cuba.
Silaha zaidi ya elfu nane na risasi zaidi ya milioni moja na laki tatu zimekusanywa
Akiwa pamoja nae,rais Santos ameifunga kwa kufuli kontena ya mwisho iliyoondoka , katika eneo la Pondores, mojawapo ya maeneo 26 ambako wanamgambo wa FARC walikusanywa na kuwa chini ya usimamizi wa umoja wa Mataifa katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
Takriban wanamgambo 7000 wa zamani wa FARC kuanzia wanaume, wanawake mpaka watoto wadogo wamesalimisha silaha zao zitakazoteketezwa katika maeneo matatu yaliyotengwa moja mjini Bogota, jengine mbele ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New-York na la tatu mjini Havana, mji mkuu wa Cuba.
Mkuu wa tume ya Umoja wa mataifa Jean Arnault amesifu zoezi lote la kukusanya silaha. Ameongeza kusema wamekusanya silaha zote 8.111, risasi milioni moja na laki tatu pamoja na kufichuliwa ghala 873 zilizokuwa na silaha 795, tani 22 za baruti, maguruneti 3957 na mabomu yanayofichwa chini ya ardhi.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef