Ugiriki yaridhia makubaliano ya mipaka ya bahari na Misri
28 Agosti 2020Makubaliano hayo yamefikiwa muda mfupi baada ya Uturuki kusogeza operesheni zake za utafiti Mashariki mwa Bahari ya Mediterrania, na kusema itafanya luteka za kijeshi katika eneo hilo wiki ijayo.
Makubaliano kati ya Ugiriki na Misri yamechukuliwa na wengi kama jibu la makubaliano yanayopingwa kati ya Uturuki na serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa, yaliochochea mzozo katika kanda ya Mediterania. Mzozo kati ya Ugiri na Uturuki umepamba moto mnamo wiki za hivi karibuni baada ya Uturuki kupeleka meli ya utafiti ya Oruc Reis, kuchunguza sakafu ya bahari katika eneo hilo, ikisindikizwa na meli za kivita.
Serikali ya Ugiriki imesema meli hiyo inaendesha operesheni zake kwenye mwambao wa Ugiriki, katika eneo ambako ina haki za kipekee juu ya eneo hilo, lenye uwezekano wa kuwa na hifadhi ya gesi ya chini ya bahari, na ilituma meli za kivita pia kuangalia na kuzifuatilia meli za Uturuki.
Baada ya kura kukamilika kwa njia ya mfumo wa kielektoniki, mswada wa wizara ya mambo ya nje wa uridhiaji wa makubaliano kati ya Ugiriki na Misri kwa ajili ya kubainisha ukanda wa kipekee kati ya mataifa hayo umepita kwa wingi mkubwa.
Mataifa huwa na haki ya kufanya utafiti wa raslimali katika maeneo yake ya baharini. Eneo la Mashariki mwa Mediterania linaaminika kuwa na akiba kubwa ya gesi na mafuta ambayo haijagunduliwa.
Makubaliano sawa kati ya Italia na Ugiriki yaliidhinishwa pia siku ya Jumatano. Msemaji wa serikali ya Ugiriki Setelios Petsas, alisema hapo jana kwamba kuridhiwa kwa makubaliano hayo kulikuwa jambo la dharura kwa kuzingatia kile alichokiita shughuli za Uturuki zinazovunja sheria.
Uturuki na Ugiriki, zote zikiwa wanachama wa jumuiya ya kujihami NATO, zinazozana kuhusu haki juu ya rasilimali za mafuta na gesin inayodhaniwa kuwepo katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterrania, kwa msingi wa madai kinzani juu ya ukubwa wa miambao yao ya bara.
reuters,afp