1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUgiriki

Ugiriki yaendelea kusaka manusura wa boti iliyozama

15 Juni 2023

Wakoaji nchini Ugiriki wanaendelea na operesheni kubwa baharini kujaribu kuwatafuta manusura wa mkasa wa kuzama kwa boti

https://p.dw.com/p/4SbbL
Griechenland | Schiffsunglück bei Kalamata
Picha: Stelios Misinas/REUTERS

Wakoaji nchini Ugiriki wanaendelea na operesheni kubwa baharini kujaribu kuwatafuta manusura wa mkasa wa kuzama kwa boti uliotokea jana na ambao hadi sasa umesababisha vifo vya wahamiaji 79.

Mapema leo asubuhi walinzi wa pwani ya Ugiriki walitia nanga kwenye bandari ya mji wa Kalamata kushusha miili iliyoopolewa baharini pamoja na wale walionusurika ambao idadi yao inafikia watu 104.

Ripoti zinasema mamia ya watu walikuwemo ndani ya boti ya uvuvi iliyozama katika maji ya kina kirefu kiasi umbali wa kilometa 80 kutoka mji wa mwambao wa Pylos.

Inaarifiwa mkasa wa kuzama kwa boti hiyo unaotajwa kuwa ndiyo mbaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni barani Ulaya, ulitokea mbele ya macho ya walinzi wa pwani ya Ugiriki.

Maafisa wa serikali mjini Athens wamesema wahamiaji hao inaoaminika walianza safari yao nchini Libya walikataa kupatiwa msaada.