Ugiriki yaanza kuwarejesha wahamiaji Uturuki
4 Aprili 2016Kundi la kwanza la wahamiaji hao limewasili nchini Uturuki asubuhi ya leo. Isaac Gamba anaarifu zaidi katika taarifa ifuatayo. Boti ya kwanza iliyobeba wahamiaji waliokuwa nchini Ugiriki, imewasili asubuhi hii katika bandari ya Dikili nchini Uturuki, ikisindikizwa na walinzi wa pwani ya nchi hiyo.
Boti hiyo, Nazli Jale ni moja ya mbili zenye kupeperusha bendera ya Uturuki, ambazo zimeondoka alfajiri ya leo jumatatu tarehe 04.04.2016 katika kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos zikiwa zimewabeba wahamiaji 131.
Mabasi yatumika kuwarejesha wahamiaji Uturuki
Mabasi maalumu kwa ajili ya kuwabeba mamia ya wahamiaji hao kwa ajili ya kusafirishwa kupelekwa nchini Uturuki nayo pia yaliwasili katika bandari za Lesbos na Chios nchini Ugiriki mapema asubuhi. Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Efkan Ala amesema nchi yake iko tayari kuwapokea watu 500 ingawa serikali ya ugiriki imetoa majina ya watu 400 tu . Hata hivyo idadi hiyo inaweza kubadilika.
Baadhi ya wahamiaji wawasilisha maombi ya hifadhi katika dakika za mwisho.
Chanzo cha kipolisi kutoka katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki ambacho kimekuwa njia kuu ya watu wanaotafuta hifadhi barani ulaya wakitokea nchini Uturuki kimesema kumekuwepo na harakati katika dakika za mwisho za maombi ya watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa barani ulaya miongoni mwa wahamiaji 3,300 walioko nchini humo.
" Tuna idadi ya zaidi ya watu 2,000 ambao tayari wameonesha nia ya kutafuta hifadhi ya kisiasa na tunahitaji kuona utaratibu unaofaa kwa ajili ya kushughulikia suala hilo'' amesema Boris Cheshirkov ambaye ni msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi katika kisiwa cha Lesbos, na kuongeza kuwa shughuli hiyo itafanyika kulingana na taratibu zinazohusiana na masuala ya hifadhi ya kisiasa nchini Ugiriki kwa wale ambao wanahitaji kuelezea juu ya kuwepo na haja ya kulindwa.
Wahamiaji hao pia wanatarajiwa kusafirishwa kurejeshwa nchini Uturuki kutoka katika visiwa vingine ambavyo pia vimeshuhudiwa kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji, kama vile Chios ambako maafisa wa shirika la kulinda mipaka ya Umoja wa Ulaya walionekana kuwasili hapo jana.
Idadi kamili ya wahamiaji wanaotarajiwa kurejeshwa Uturuki haijawekwa wazi
Hata hivyo maafisa wa serikali ya ugiriki hadi sasa hawajaweka wazi kuhusiana na idadi kamili ya wahamiaji watakaorejeshwa nchini Uturuki katika utekelezaji wa makubaliano hayo ingawa shirika la habari la nchi hiyo limekaririwa katika taarifa yake likisema kuwa kiasi ya wahamiaji 250 kutoka Bangladesh, Pakistan, Sri Lanka na kutoka mataifa ya Afrika watakuwa wakirejeshwa kila siku kati ya siku za Jumatatu na Jumatano.
Yiorgos Kyritsis, msemaji wa kitengo kinachoratibu masuala ya wahamiaji nchini Ugiriki, amesisitiza kuwa operesheni ya jumatatu tarehe 04.04.2016 itawahusu wale tu ambao hawajawasilisha maombi ya kuomba hifadhi ya kisiasa.
Makundi ya haki za binadamu yakosoa hatua hiyo.
Makundi ya haki za binadamu tayari yamekosoa makubaliano yanayohusu kurejeshwa kwa wahamiaji hao, yaliyofikiwa kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya, yakihoji kama yamefuata sheria na pia kuzingatia maadili.
"Hatujui kwa kweli kipi kitatokea" alisikika Peter Sutheland ambaye ni afisa mwandamizi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi.
Makubaliano hayo yalisainiwa mwezi Machi mwaka huu mnamo wakati mataifa ya ulaya yakikabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia huku zaidi ya wakimbizi milioni moja wakiwasili barani humo kutoka katika mataifa ya Mashariki ya Kati na kwingineko katika kipindi cha mwaka jana.
Chini ya makubaliano hayo Uturuki iliahidiwa kupata msaada zaidi wa kifedha na raia wake kusafiri bila viza katika mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/RTRE
Mhariri: Daniel Gakuba