1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki bado haijampata Rais mpya

Abdu Said Mtullya29 Desemba 2014

Baada ya Bunge kushindwa kwa mara ya tatu kumchagua Rais, Ugiriki itaitisha uchaguzi wa mapema mwezi ujao.Pana hofu huenda chama kinachopinga sera ya kubana matumizi kikashinda katika uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/1EC6F
Waziri Mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Antonis SamarasPicha: picture alliance/AA/A. Mehmet

Uchaguzi huo ambao Waziri Mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras amependekeza ufanyike tarehe 25, ya mwezi Januari huenda ukautikisa uchumi na masoko ya fedha baada ya hali mbaya ya kifedha ya Ugiriki kukaribia kuuvuruga ukanda wote wa sarafu ya Euro mnamo mwaka wa 2012,

Hisa za Ugiriki zilipoteza thamani kwa asilimia zaidi ya 7 baada ya bunge leo kushindwa kwa mara ya tatu kumchagua Rais. Hapa awali hisa hizo zilishuka kwa asilimia 11 katika muktadha wa hofu juu ya chama cha mrengo wa shoto,Syriza kuweza kuyabatilisha mageuzi mengi ya kiuchumi, ikiwa kitashinda katika uchaguzi wa tarehe 25 mwezi wa Januari.

Mjumbe serikali Stavoros Dimas hakuweza kupata idadi ya kura zilizohitajika. Badala ya kura 180 alipata 168 tu. Na kwa mujibu wa katiba ya Ugiriki Bunge linapaswa kuvunjwa mnamo kipindi cha siku 10.

Waziri Mkuu Antonis Samaras amesema amemwomba Rais anaemaliza muda wake, Karolos Papoulias aitishe uchaguzi tarehe 25 ya mwezi ujao.

Chama cha Syriza chapinga sera za kubana matumizi

Mwenyekiti wa chama cha upinzani Alexis Tsipras alieleza wazi kabla ya Bunge kupiga kura kwamba chama chake Syriza kinaipinga siyo tu serikali ya Ugiriki bali pia kinawapinga wanasiasa muhimu sana wa Umoja wa Ulaya.

Mwenyekiti huyo amesema Bibi Merkel na bwana Schäuble wanajifanya kana kwamba hawasikii. Lakini amesema ukweli utawaacha nyuma. Ameeleza kuwa Ukanda wa Euro hauwezi daima kujiweka katika mazingira tete.

Bwana Tsipras aliwaambia waandishi wa habari kwamba,katika msingi wa utashi wa wananchi, makubaliano yaliyofikiwa hapo awali juu ya sera ya kubana matumizi hayatakuwa na maana tena. Bwana Tsipras amesema mustakabal umeshaanza nchini Ugiriki. Kura za maoni zinaonyesha kwamba mfungamano wa vyama unaoongozwa na Waziri Mkuu Samaras upo nyuma ya chama cha upinzani,Syriza.

Athari za matokeo ya kura zaonekana

Athari za matokeo ya kura ya leo bungeni zimeanza kuonekena. Kiwango cha malipo kwa ajili ya dhamana za Ugiriki zenye muda wa miaka 10, pia kilipanda hadi kufikia asilimia 9.55 kutoka kiwango cha asilimia 8.5 cha wiki iliyopita.

Benki Kuu ya Ulaya,ECB imesema leo kwamba itawasiliana na viongozi wa Ugiriki ili kupata mapendekezo yao juu ya kuendelea na mchakato wa kuzitathmini hatua za kuiokoa Ugiriki, baada ya wabunge kushindwa kumpata Rais mpya. Katika tamko lake Benki hiyo imesema kwamba ni juu ya wapiga kura wa Ugiriki wenyewe kuamua juu ya bunge na serikali yao. Benki hiyo imesema haitajiingiza katika mchakato wa kidemokrasia wa nchini humo.

Hata hivyo wataalamu wamesema pana asilimia karibu 30 ya uwezekano wa Ugiriki kutumbuki katika mgogoro mwingine mkubwa sana.

Mwandishi:Mtullya abdu/rtre/ZA.

Mhariri: Iddi Ssessanga