1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaUganda

Uganda yapokea chanjo ya Ebola kwa kirusi aina ya Sudan

8 Desemba 2022

Shirika la Afya duniani WHO pamoja na serikali ya Uganda leo wamezindua chanjo ya majaribio dhidi ya virusi vya aina ya Sudan vya ugonjwa wa Ebola.

https://p.dw.com/p/4Kg88
Uganda Battles Seventh Ebola Outbreak Since 2000
Picha: Luke Dray/Getty Images

Chanjo hiyo itatolewa kwa watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo chini ya mradi ujulikanao kama ‘tokomeza Ebola'.

Haya yanafanyika wakati ambapo waziri wa afya wa Uganda Jane Ruth Aceng amefahamisha kuwa katika muda wa siku tisa sasa hakujakuwepo na mgonjwa mpya wa Ebola.

Shehena ya kwanza ya chanjo elfu moja mia mbili imekabidhiwa wizara ya afya na wataalamu wameeleza kuwa wamejiandaa kuwachoma chanjo hiyo watu wanaojitolea kwa hiari. Miongoni mwa hatua watakazochukua ni kuwaelezea kuhusu usalama wa chanjo hiyo.

Tangu kuzuka kwa mripuko wa Ebola Uganda mwezi Septemba mwaka huu, wanasayansi wamekuwa mbioni kutafuta chanjo inayoweza kudhibiti aina hiyo ya kirusi cha Ebola kijulikanacho kama Sudan.

Chanjo hiyo inaoyanza kufanyiwa majaribio ni moja kati ya chanjo tatu zilizopendekezwa baada ya kufanyiwa majaribio ya awali.