1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yafunga kazi za mashirika 54 yasiyo ya kiserikali

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
20 Agosti 2021

Serikali ya Uganda imeamua kusitisha shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali 54 nchini humo. Shirika moja kati ya hayo yaliyosimamishwa limesema uamuzi huo wa serikali ya Uganda ni hujuma za kisiasa.

https://p.dw.com/p/3zH6X
Uganda Ölförderung Umwelt Indigene Total
Picha: Jack Losh

Miongoni mwa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yaliyoathiriwa ni pamoja na yale ya misaada ambayo yanafanya kazi ya kuwatetea wanaharakati wa kisiasa na watu walioathiriwa na mradi wa uzalishaji mafuta ghafi mradi ulikoko magharibi mwa Uganda jambo ambalo limewakera baadhi ya maafisa wa serikali.

Mkuu wa Taasisi ya Utawala wa mswala ya Nishati (AFIEGO) kanda ya Afrika, Dickens Kamugisha amesema hatua hii ni ya kisiasa na kwamba mtu mara moja unakua adui mkubwa wa serikali ya Uganda pale atakapojihusisha na kazi ambazo haziipendezi serikali lakini amesema watapeleka malalamiko yao mahakamani kupinga uamuzi huo wa serikali.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: Tanzania State House/Xinhua News Agency/picture alliance

AFIEGO inahusika katika kutetea haki za watu walioathiriwa na mradi wa maendeleo ya uzalishaji wa mafuta ambayo hayajasafishwa. Taasisi hiyo na nyinginezo za kutoa misaada zilizofungiwa zimekuwa zikiendesha kampeni kupinga mapendekezo ya mradi huo wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), wakisema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea athari katika mazingira.

Hata hivyo mwenyekiti wa Bodi inayosimamia mashirika yasiyo ya kiserikali inayoendeshwa na serikali, Steve Okello, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba amri ya kusimamishwa mashirika hayo imetolewa kwa kuzingatia sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kutofuata kanuni ambazo zinakataza mashirika yasiyo ya kiserikali kujihusisha na siasa. Serikali ya Rais Yoweri Museveni kwa miaka kadhaa imekuwa ikiongeza shinikizo kwa mashirika yasiyo ya kiserikali akiyatuhumu baadhi ya mashirika hayo kwa kuunga mkono upinzani.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Chapter Four Uganda, Nicholas Opiyo
Mkurugenzi wa Taasisi ya Chapter Four Uganda, Nicholas OpiyoPicha: CHAPTER FOUR UGANDA/REUTERS

Mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita, polisi walimweka kizuizini mkosoaji wa serikali ambaye ni mkuu wa shirika la Chapter Four Uganda, kwa tuhuma za kufanya utapeli wa pesa. Shirika hilo ni mojawapo kati ya mashirika yaliyofungiwa leo. Shirika lake limekanusha madai hayo dhidi ya mkurugenzi wake likisema kukamatwa kwake ni sehemu ya kuwakandamiza wapinzani.

Chapter Four for Uganda ni shirika la uangalizi wa uhuru na haki za kiraia ambalo limekuwa likiendehsa harakati za kuwatetea viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani wanaozuiliwa wakati wanakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na siasa.  

Rais Yoweri Museveni, ambaye ametawala Uganda tangu mwaka 1986, kwa muda mrefu amekuwa analaumiwa na serikali za magharibi, makundi ya kimataifa na pia upande wa upinzani nchini humo kwa kuvitumia vikosi vya usalama kuwatisha na kuwasumbua wapinzani, wakosoaji na wanaharakati wanaotetea haki.

Vyanzo:/RTRE/AFP