1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yaanza kuomboleza kifo cha Rais Magufuli

Lubega Emmanuel19 Machi 2021

Uganda imeanza rasmi kuomboleza kifo cha rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kufuatia agizo la rais Yoweri Museveni kwamba pia bendera zote nchini zipeperushwe nusu mlingoti hadi siku ya maziko.

https://p.dw.com/p/3qsKb
Tansania Chato 2020 | Yoweri Museveni, Präsident Uganda
Picha: Tanzania State House/Xinhua News Agency/picture alliance

Wakati huohuo, wanasiasa wa Uganda wamesifu mchakato wa amani wa kupokezana madaraka ambao umeshuhudiwa hii leo wakati mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kuwa rais wa Tanzania.

Bendera zote nchini Uganda zimepeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya maombolezo ya rais John Pombe Magufuli wa Tanzania.

Hii ni baada ya agizo la rais Yoweri Museveni siku ya Alhamisi jioni ambapo  kwa mara ya kwanza alitoa tamko rasmi kuhusu kifo cha kiongozi huyo wa awamu ya tano Tanzania.

Alimtaja hayati Magufuli kuwa kiongozi aliyekuwa na uzalendo halisi wa Kiafrika ambaye pia alimfunza kuhusu njia bora za kupambana na vitendo vya ulaji rushwa.

Katika bunge la Uganda, spika Rebecca Kadaga amewaongoza wabunge kutoa rambirambi zao kwa wananchi na serikali ya Tanzania. 

Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa Rais John Pombe Magufuli aliaga dunia tarehe 17.03.2021
Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa Rais John Pombe Magufuli aliaga dunia tarehe 17.03.2021Picha: Sadi Said//REUTERS

Wamelezea furaha yao kwamba Tanzania inaendelea kuwa mfano wa kuigwa wa demokrasia pale inapozingatia katiba yake na kuendesha mchakato wa kupokezana madaraka kwa amani na ustaarabu wa juu.

Kuapishwa kwa mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa rais hii leo nalo ni  jambo ambalo limewafurahisha watu wengi nchini Uganda.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi kwenye mpaka wa Uganda na Tanzania kule Mutukula wanahofia kuwa baada ya kifo cha rais Magufuli, viongozi wa eneo hilo huenda wakaanza kuwanyanyasa kwa kuwanyima uhuru raia wa pande zote mbili kuendesha shughuli zao kama walivyoafikiana marais hao walipokutana hapo mwaka 2017.

Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii,  kitabu cha salamu za rambirambi kilikuwa bado hakijafunguliwa kwenye ubalozi wa Tanzania.