Uganda: Polisi yasitisha mikutano ya siasa ya Bobi Wine
14 Septemba 2023Tangu mwanzo, fursa ya nadra aliyopewa kiongozi huyo wa upinzani kuendesha mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini Uganda iliwashangaza wengi.
Rais wa chama kikuu cha upinzani Robert Kyagulanyi yaani Bobi Wine alianza mikutano hiyo katika eneo la kusini magharibi mwa Uganda ambayo ni ngome kuu ya rais Yoweri Museveni hasa kutokana na kwamba yeye ni mzawa wa eneo hilo la Ankole.
Soma pia:Bobi Wine azinduwa maandalizi kuelekea uchaguzi wa 2026
Hata hivyo Bobi Wine nae anayo nasaba katika eneo hilo kutokana na mke wake anatoka jamii hiyo, alivutia umati mkubwa wa watu katika mikutano yake huko na sehemu zingine za nchi bila kutatizwa na polisi.
Hata hivyo mambo yalianza kumwendea vibaya kufuatia matamshi yaliofasiliwa kueneza chuki za kikabila hasa dhidi ya watu wa jamii ya Ankole.
Alikosolewa na watu mbalimbali kwa matamshi hayo na polisi ikatoa taarifa kuwa ingechunguza matamshi hayo na ingemfungulia mashtaka.
Polisi kusitisha mikutano ya Bobi wine
Hapo jana polisi iliagiza mikutano hiyo kusimamishwa. Msemaji wa polisi Fred Enanga aliwaambia waandishi wa habari kwamba mikutano yote ya uhamasishwa imesitishwa mara moja.
Hata baada ya kutishiwa kuwa angekamatwa kutokana na matamshi yake, Bobi Wine aliwataka polisi wathubutu kumkamata kwa matamshi hayoakisema afadhali yeye ambaye hutamka tu kuhusu ukabila tofauti na rais Museveni ambaye huonyesha waziwazi mapendeleo na ubaguzi wa kikabila.
"Tunaendelea kuhamasisha watu kwa idhini au bila ya idhini ya Museveni." alisema Bobi wine.
Hapo jana Bobi Wine alikamilisha awamu ya kwanza ya mikutano hiyo mjini Arua kaskazini magharibi mwa Uganda.
Soma pia:Kyagulanyi na Besigye kuungana na vyama vingine vitatu
Mikutano hiyo ilienda sambamba na chama chake cha NUP kufungua rasmi ofisi zake sehemu hizo na kuwatambulisha viongozi wa mashinani wa chama hicho kwa wananchi.