Ugaidi wa kuvuka mipaka kitisho cha Afrika
26 Juni 2014Rais huyo ametoa onyo hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa kilele wa Umoja wa Afrika unaofanyika mjini Malabo huko Guinea ya Ikweta ambapo suala kuu ni kupambana na ugaidi.
"Afrika inakabiliwa na kitisho cha magaidi wanaovuka mipaka" Alisema al-Sisi na kutoa wito kwa viongozi hao wa Afrika waliokusanyika katika mji mkuu wa Guinea ya Ikweta kuunganisha nguvu katika kukabiliana na kitisho hicho kwa lengo la kulinda utu wa watu wake na uchumi kwa ujumla.
Al-Sisi ambae kuhudhuria kwake katika mkutano huo kunalirejesha taifa hilo katika ramani ya siasa za Afrika alisisitiza kitisho hicho cha ugaidi kinahitaji nguvu za pamoja. Misri ilisimamishwa uanachama wake katika umoja huo baada ya kumuondoa Mohammed Mursi, wakati rais huyo wa sasa akiwa mkuu wa majeshi wa taifa hilo.
Ongezeko la makundi ya wenye misimamo mikali
Mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika katika taifa hilo dogo lenye utajiri wa mafuta umegubikwa sana na suala la kuongezeka kwa makundi ya waislamu wenye misimamo mikali ambayo wamekuwa wakifanya mashambulizi karibu kila siku barani humo.
Mkutano huu wa sasa unafanyika katika mji uitwao Sipopo ambako kumejengwa majunga mahususi kwa ajili ya marais 52. Majengo hayo yalijengwa kwa ajili ya mkutano kama huo uliopita wa 2011 na rais Teodoro Obiang Nguema.
Jitahada ya kuunda jeshi la Umoja wa Afrika
Siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo, maafisa waandamizi wa umoja huo walisema bara hilo linapiga hatua katika uundwaji wa jeshi la pamoja-African Standby Force (ASF) ambalo linapaswa kuwa tayari itakapofikia mwishoni mwa mwaka ijao wakati huu ambao viongozi wake wakitaka kuwepo kwa utegemezi mdogo kwa majeshi kutoka nje ya bara hilo.
Kuchelewa kuundwa kwa jeshi hilo kulilazimisha mataifa ya Afrika kuiomba Ufaransa kuingilia kijeshi katika mataifa ya Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka uliopita kwa lengo la kukabiliana na mizozo ya mataifa hayo. Smail Chergui, kamishna wa amani na ulinzi wa Umoja wa Afrika alisema vikosi vinne kati ya vitano vinavyounda jeshi zima la kanda hiyo viko tayari ikiwemo kikosi cha Afrika Kaskazini.
Katika mkutano huo ambao uliadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa baraza la Baraza la Usalama na Ulinzi la Umoja wa Afrika amesema hatua zimepigwa katika uundwaji wa jeshi hilo na kwamba operesheni zake zinatarajiwa kuanza rasmi mwaka 2015.
Umuhimwa migogoro kwa viongozi wa Afrika
Akizungumza kwenye mkutano huo jana, Rais wa Chad Idriss Deby alisema mfululizo wa migogoro barani Afrika kuanzia Sudan Kusini mpaka Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mambo yanayowakumbusha viongozi wa Afrika kwamba bara hilo linahitaji kufanya jitihada zaidi kuimarisha taasisi zake za usalama.
Guinea ya Ikweta, kama taifa lililo kusini mwa jangwa la Sahara ambalo linashikilia nafasi ya tatu katika uzalishaji wa mafuta barani Afrika kwa hivi sasa limegubikwa na tuhumua za ukiukwaji wa haki za binaadamau na wanasiasa waliobobea kuhodhi utajiri wake.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP/RTR
Mhariri: Mohammed Abdulrahman
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman