Ufaransa yakumbuka miaka 75 ya mauaji ya Wayahudi
16 Julai 2017Rais wa Ufansansa Emmanuel Macron Jumapili (16.07.2017) amekuwa na kumbukumbu ya miaka 75 tokea kukusanywa na kukamatwa kwa Wayahudi 13,000 ili kupelekwa kwenye makambi ya kifo ya Wanazi na kukiita kitendo cha kuwajibika kwa Ufaransa kuwa ni "ukweli mtupu" katika tukio lililohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Akizungumza karibu na uwanja wa Velodrome d' Hiver ambapo Wayahudi walihamishwa mwaka 1942 Macron amesema "Ni Ufaransa kweli ambayo uliyoandaa kuwakusanya Wayahudi hao na kwamba hakuna Merumani hata mmoja alieshiriki."
Kuwepo kwa Netanyahu kwenye tukio hilo kumezusha utata ambapo chama cha Wafaransa wenye asili ya Kiyahudi kwa ajili ya amani (UJFP) kimeuita mwaliko huo kuwa "fadhaa" na "haukubaliki".
Chama hicho kimeishutumu serikali ya Israel kwa kutumia kumbukumbu ya wahanga wa Wanazi kuwafanya watu waamini kwamba Israel inawakilisha Wayahudi wote duniani.
Hafla hiyo inakumbuka siku ambapo maafisa wa serikali ya utawala huo wa Vichy katika Ufaransa iliokuwa ikikaliwa kwa mbavu na Wanazi ulipoanza kuwakusanya na kuwakamata Wayahudi 13,152 na kuwapeleka uwanja wa Vedrome d' River mjini Paris.
Abeba lawama
Hawapindukii 100 ya wale waliopelekwa katika uwanja huo na baadae kupelekwa kwenye makambi ya kifo ya Wanazi waliweza kunusurika.
Macron ni rais wa nne wa Ufaransa kukubali lawama kwa dhima iliyotimiza Ufaransa katika kuwasafirisha Wayahudi hao kwenye makambi ambapo jumla yake wanafikia 75,000 tokea Jacques Chiraq alipokiri hayo mara ya kwanza hapo mwaka 1995.Macron amesema "Wakati hufanya kazi yake.Kumbukumbu zinafunguliwa na ukweli unajitokeza.Ni ukweli kabisa, usiotenguka.Unajiweka kwetu sote."
Netanyahu amesifu "ushujaa maalum " wa upinzani wa Ufaransa kwa Manazi na kusifu raia wa Ufaransa wenye heshima ambao walihatarisha maisha yao wenyewe kuwaokowa maelfu zaidi ya Wayahudi kuungamia katika mkambi hayo ya kifo ambapo takriban milioni sita wangelikufa kwa jumla kati ya mwaka 1941 na mwaka 1945.
Amesema kwa "heshima takatifu ya wale walioangamia ....tukumbuke kipindi kilichopita na tuhakikishe usalama wa kipindi cha kesho."Ameongeza kusema nguvu ya Israel ni hakikisho moja la uhakika kwamba wananchi ya Kiyahudi katu hawatokabiliwa tena na Holocaust(maangamizi ya Wayahudi).
Netanyahu akosolewa
Miongoni mwa wale waliomkosowa Netanyahu kwa uwepo wake ni balozi wa zamani wa Ufaransa kwa Israel Elie Barnavi alieliambia shirika la habari la AFP kwamba imemfanya akose raha kidogo.Ameongeza kusema "hadithii hii hauhusiani na Israel."
Netanyahu anatarajiwa kumshawishi Macron aachane na msimamo wake kuhusu mzozo kati ya Wapalestina na Israel.
Lakini bado hajulikani iwapo kiongozi huyo atafuata msimamo wa kujihusisha zaidi wa mtangulizi wake Francois Hollande ambaye juhudi zake za kuiandaa jumuiya ya kimataifa katika suala hilo umezighadhibisha Usrael.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri. Isaac Gamba