Ufaransa yaapa kuimarisha usalama baada ya mwanafunzi kuuawa
25 Septemba 2024Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bruno Retailleau ameapa leo kuchukuliwa kwa hatua baada ya mwanamume mmoja raia wa Morocco anayeshukiwa kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 19 na kuuacha mwili wake kwenye msitu mmoja mjini Paris kukamatwa nchini Uswisi.
Chanzo kinachofahamu kisa hicho na kilichozungumza na shirika la habari la AFP, kilimtaja mshambulizi huyo kuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 22 mwenye asili ya Morocco.
Waendesha mashtaka wamesema mshukiwa huyo awali alikuwa amehukumiwa kwa kosa la ubakaji na alikuwa chini ya amri ya kuondoka Ufaransa. Soma: Ufaransa yafunga viwanja 8 vya ndege ikihofia ugaidi
Mauaji ya mwanafunzi huyo yanatarajiwa kuzidisha mvutano wa kisiasa nchini Ufaransa ambapo serikali mpya ya mrengo wa kulia imepanga kukabiliana na wahamiaji.
Retailleau amesema huo ni uhalifu wa kuchukiza. Retailleau, ambaye Jumatatu alichukua uongozi kutoka mtangulizi wake Gerald Darmanin, ameapa kuimarisha sheria na utulivu, kuimarisha sheria ya uhamiaji na kurahisisha mchakato wa kuwafukuza wageni wanaopatikana na hatia ya uhalifu.