1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaahidi kuimarisha uhusiano na Uingereza

29 Agosti 2024

Rais wa wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameahidi kuimarisha uhusiano na Uingereza katika sekta ya ulinzi na usalama, pamoja na uhamiaji na nishati.

https://p.dw.com/p/4k45T
Frankreich Wahlen Emmanuel Macron
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Ahadi hiyo ameitoa leo kufuatia mkutano wake na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer mjini Paris.

Starmer amesema wamejadiliana masuala mengi na mwenyeji wake ikiwemo umuhimu wa kupunguza mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati, wakisisitiza wito wao wa kupatikana makubaliano ya kusitisha mapigano mara moja.

''Kwa hiyo, hizo ndizo mada tulizojadiliana, kama sehemu ya kujenga upya na kuhakikisha kuwa dhamira yetu ya kwanza ambayo inakuza uchumi, ni muhimu kabisa kwa kila kitu ambacho tunakifanya,'' alisema Starmer.

Macron na Starmer pia wamekubaliana kuwa ni muhimu kuendelea kuiunga mkono Ukraine ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi hiyo, bara lote la Ulaya kwa ujumla.

Paris ni kituo cha pili cha ziara ya Starmer katika nchi muhimu za Umoja wa Ulaya, baada ya kuizuru Berlin na kutangaza mkataba wa pamoja na Kansela Ilaf Scholz.