1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yashinda Olimpiki, Ukraine waangukia pua

25 Julai 2024

Jumatano ilikuwa siku ya kwanza ya mechi za kandanda za Michezo ya Olimpiki mjini Paris ambapo wenyeji Ufaransa walipata ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Marekani.

https://p.dw.com/p/4ijA4
Wachezaji wa Ukraine na Irak wakipambana katika Olimpiki
Wachezaji wa Ukraine na Irak wakipambana katika OlimpikiPicha: Laurent Cipriani/AP Photo/picture alliance

Alexandre Lacazette aliwatia uongozini Ufaransa kisha goli lao la pili likafungwa na mchezaji mpya wa Bayern Munich Michael Olise kisha Loic Bade akafunga la tatu na hatimaye hao wenyeji wakapata ushindi muhimu katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa mjini Marseille.

Mapema Jumatano Morocco ilipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Argentina katika mechi iliyosimamishwa kwa kipindi cha takriban saa 2 kwa kuwa mashabiki waliuvamia uwanja katika dakika za mwisho za mechi.

Uhispania wao walikuwa wanachuana na Uzbekistan na waliishia kupata ushindi wa 2-1 katika mpambano wa kundi C. Mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Parc des Princes mjini Paris iliwavutia jumla ya mashabiki 35,000.

Mwakilishi wa Afrika Guinea alikuwa anacheza na New Zealand na hakufua dafu kwani alifungwa 2-1 mjini Nice katika mechi ya pili ya kundi A. Misri na Jamhuri ya Dominica wao waliishia kugawana pointi kwa kuwa mchuano wao ulimalizika 0-0 huko Nantes.

Japan ndio waliovuna ushindi mkubwa kwa siku ya Jumatano kwani waliwalemea paraguay 5-0 Shunsuke Mito na Shota Fujio wote wakipata mabao mawili katika mechi hiyo ya kundi D.

Irak nao walipata ushindi muhimu wa 2-1 walipokuwa wakikwaana na Ukraine kisha Mali wakatoka sare ya 1-1 na Israel.