Udugu wa Kiislamu wabanwa zaidi
26 Septemba 2013Katika taarifa yake iliyotolewa leo (25.09.2013) katika mtandoa wa facebook, chama cha Udugu wa Kiislamu kimesema "Sisi waandishi habari wa gazeti la Uhuru na Haki tunalaani kitendo cha vikosi vya usalama kufunga makao makuu ya gazeti".
Usiku wa kuamkia leo, jeshi la polisi lilizishambulia ofisi hizo na kuondoa nyaraka kadhaa zilizokuwemo. Chanzo kimoja kutoka katika kitengo cha usalama cha Misri kimesema hatua hiyo inatokana na uamuzi wa mahakama wa Jumatatu, wa kupiga marufuku chama hicho na kuamuru kudhibitiwa hazina yake.
Vurugu ni sababu za operesheni
Akiendeleza kutoa ufafanuzi kuhusu namna wanavyoendesha operesheni hiyo chanzo hicho kimesema uamuzi wa mahakama ambao umesababasha kutekelezwa kwa hatua hiyo kunatokana na kuwepo kwa mashitaka ya kuchochea vurugu pamoja na vitendo vya ugaidi kulikoteka katika siku za hivi karibuni.
Mwezi Julai mwaka huu, jeshi lilimuondoa madarakani rais Mohamed Mursi ambapo pia chama chama chake cha Udugu wa Kiislamu kimeshuhudia mikasa ya mamia ya wanachama wake kuuwawa na wengine maelfu kukamatwa tangu wakati huo.
Waandishi 50 wawakwepa polisi
Kampeni hii ya sasa ya vikosi vya usalama imelazimisha vilevile zaidi ya waandishi habari 50, ambao wanafanikisha uchapishaji wa kila siku wa gazeti hilo "Uhuru na Haki" kufanya kazi kwa kujificha kwa lengo la kukwepa kutiwa mbaroni.
Jina la gazeti hilo limetolewa na tawi moja la kisiasa la chama cha Udugu wa Kiislamu kikiwa na shabaha ya kufanya harakati za kumrejesha madarakani Mohamed Mursi, baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya kiongozi huyo aliyechaguliwa kidemokrasia.
Chama cha Udugu wa Kiislamu kiliibuka kutoka gizani na kushinda katika chaguzi na bunge na rais baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa kiimla Hosni Mubarak kufuatia vuguvugu la mwaka 2011 nchini humo.
Idadi kubwa ya Wamisri waligawanyika baada ya Mohamed Mursi kujilimbikizia madaraka na kushindwa kuukwamua uchumi na kuwafanya waingie mitaani kumpinga, jambo ambalo pia lilisababisha jeshi kuingilia kati. Wengi wa raia hao kwa hivi sasa wanamtukuza kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Sisi kutokana na hatua ya kufanikishwa kuondolewa madarakani Mohamed Mursi.
Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Josephat Charo