1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa chanzo cha mauaji ya Rwanda wakamilika

22 Desemba 2017

Majaji wa kukabiliana na ugaidi wamekamilisha uchunguzi wao wa lile shambulizi la kombora lililosababisha mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

https://p.dw.com/p/2pojD
Symbolbild - Ruanda Opfer des Bürgerkriegs
Picha: Getty Images/C. Somodeville

Kulingana na duru za kisheria, majaji hao sasa wataamua iwapo wafungue mashtaka kuhusiana na kesi hiyo.

Kombora hilo lililoishambulia ndege karibu na uwanja wa ndege wa Kigali Aprili mwaka 1994, lilimuua rais Juvenal Habyarimana na kuzusha umwagikaji wa damu kwa siku mia moja na kuwaacha karibu watu 800,000 wakiwa wamefariki dunia, wengi wao kutoka kabila dogo la Watutsi.

Mauaji hayo ya halaiki kwa miongo miwili sasa yamesababisha hali ya taharuki kati ya Ufaransa na Rwanda, huku Rwanda ikiituhumu Ufaransa kwa kuhusika katika mauaji hayo, kupitia kukiunga mkono na kukipa mafunzo ya kijeshi kikosi cha Wahutu cha Habyarimana ambacho kilifanya mauaji mengi nchini humo.

Majaji hao sasa watasubiri maoni ya afisi ya kiongozi wa mashtaka wa Ufaransa

Uchunguzi huo wa Ufaransa kuhusiana na shambulizi hilo, ulioanzishwa mwaka 1998 kwasababu waliokuwa katika ndege hiyo walikuwa Wafaransa unawaelekezea lawama waasi wa Kitutsi walioongozwa na rais wa sasa wa Rwanda Paul Kagame.

Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Picture alliance/AP Photo/E. Murinzi

Watutsi 7 wamefunguliwa mashtaka bila uwepo wao na majaji hao wa Ufaransa na miongoni mwao ni waziri wa ulinzi wa sasa James Kabarebe na Franck Nziza anayedaiwa kufyatua kombora hilo.

Kwa kuwa wameshakamilisha uchunguzi wao, majaji hao sasa watasubiri maoni ya afisi ya kiongozi wa mashtaka wa Ufaransa iwapo kufunguliwe mashtaka halafu wafanye uamuzi wa mwisho katika tarehe ambayo haijawekwa wazi.

Serikali ya Rwanda imekuwa ikiwalaumu Wahutu walio na itikadi kali kwa kuuwawa kwa Habyarimana ikisema kwamba walikuwa wanataka kumuondoa rais huyo ambayo walikuwa wanamchukulia kama aliye na msimamo wa kadri.

Uhusiano wa kidiplomasia ulivunjika kabisa kati ya Rwanda na Ufaransa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2006 pale Ufaransa ilipotaka washukiwa 9 wakamatwe, wakiwemo 7 ambao tayari wameshafunguliwa mashtaka.

Majaji hao walitaka kumdadisi Faustin Kayumba Nyamwasa

Uhusiano ulianza kuwa mzuri taratibu hadi ilipofikia mwaka 2014 pale majaji wa Ufaransa waliposema kwa mara ya kwanza kwamba wamekamilisha uchunguzi wao. Lakini kulizushwa hali ya taharuki tena mwaka huo huo pale rais Paul Kagame aliporejelea kuwatuhumu wanajeshi wa Ufaransa walihusika katika mauaji hayo ya halaiki na Oktoba mwaka jana, uhusiano ukapwaya tena pale majaji hao wanahusika na uchunguzi walipouanzisha tena.

Ruandischer Dissident Faustin Kayumba Nyamwasa
Majaji hao walitaka kumdadisi Faustin Kayumba NyamwasaPicha: STEPHANE DE SAKUTIN/AFP/GettyImages

Walisema wanataka kumdadisi mtu anayempinga rais Kagame, Faustin  Kayumba Nyamwasa ambaye amemlaumu rais huyo wa sasa kwa kuhusika na shambulizi hilo la kombora lakini duru zilizozungumza na shirika la habari la AFP zilisema Afrika Kusini, nchi ambayo kwa sasa inampa hifadhi, ilikataa ahojiwe kupitia video.

Wote waliokuwemo katika ndege hiyo ya Habyarimana waliuwawa na kombora hilo, akiwemo rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira, aliyekuwa anarejea nchini mwake kutoka kwenye mazungumzo ya amani nchini Tanzania.

Wakati wa shambulizi hilo, Ufaransa ilikuwa inawaunga mkono pakubwa Wahutu na ripoti mpya ilitolewa na serikali ya Rwanda mwezi huu inasema, Ufaransa ilipuuza ishara za mauaji ya halaiki zilizokuwa wazi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu