1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Angola watia fora barani Afrika

P.Martin17 Mei 2007

Barani Afrika,Angola ni mzalishaji mkuu wa pili wa mafuta kusini mwa Sahara.Baada ya kujitoa kwenye vita vya miongo kadhaa,Angola siku moja huenda ikachomoza kama dola lenye usemi mkubwa kiuchumi,kisiasa na kijeshi katika bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/CHEF
Wasaka mabomu yaliyotegwa ardhini wakati wa vita vya Angola
Wasaka mabomu yaliyotegwa ardhini wakati wa vita vya AngolaPicha: PA/dpa

Nchini Angola,vita vya kugombea uhuru wake kutoka Ureno,kati ya mwaka 1961 na 1974 na baadae vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 1975 hadi 2002 vilisababisha uharibifu mkubwa nchini humo.Vita hivyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu milioni moja na takriban milioni nne wengine walipoteza makazi yao katika nchi hiyo,kusini-magharibi ya Afrika.

Sasa lakini nchini Angola,uchumi unastawi kutokana na mauzo ya mafuta.Kwa mfano,katika mwaka 2006,uchumi wa nchi hiyo ulikuwa kwa asilimia 15 ikitarajiwa kuwa mwaka huu ukuaji huo utaongezeka kwa maradufu.

Kwa sasa,Angola ni muuzaji mkubwa kabisa wa mafuta kwa China na inashika nafasi ya saba miongoni mwa nchi zinazoiuzia mafuta Marekani. Kiasi ya mapipa milioni 1.4 ya mafuta huchimbuliwa kila siku.Mwaka huu,idadi hiyo inatazamiwa kufikia mapipa milioni 2.

Kwa mujibu wa waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Angola,Joao Baptista Ngandajina hatua zingine za kuifanya Angola kuongoza katika kanda hiyo zitachukuliwa kwa kuanzisha mradi wa nishati ya kinyuklia.Alipozungumza na waandishi wa habari alisema,licha ya kwamba Angola ni miongoni mwa wauzaji wakuu kabisa wa mafuta duniani,nchi hiyo ina kasoro katika uzalishaji wa nishati.Kwa hivyo kwanini isianze kufikiria miradi ambayo katika siku zijazo itaweza kuzalisha nishati kutokana na nguvu za kinyulia.Lakini alisisitiza kuwa mkakati huo hatohusika na utengenezaji wa silaha za nyuklia.Wakati huo huo alieleza kuwa akiba ya madini ya uranium imegunduliwa nchini Angola, lakini alikataa kueleza ni katika eneo gani.

Kwa upande mwingine,mapema mwezi huu,mtaalamu wa nishati ya nyuklia Antonio Costa e Silva alisema kuwa akiba kubwa ya madini ya uranium nchini Angola imeivutia China.Kwa maoni yake,China itajaribu kujitolea kujenga vinu vya nishati na kutoa mafunzo kwa waajiriwa wa sekta hiyo nchini Angola.

Ikiwa bunge litaidhinisha mswada wa sheria unaoandaliwa kuhusu nishati ya nyuklia,basi Angola itakuwa na ruhusa ya kuanza kuzalisha nishati ya nyuklia.

Serikali ya Rais Jose Eduardo dos Santos imeeleza kuwa mwanzoni,kipaumbele kitatolewa kwa miradi ya utafiti pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta hiyo ya nishati.