1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: CDU inao mlima wa kupanda kushinda uchaguzi ujao

Daniel Gakuba
9 Septemba 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amepuuza utabiri wa tafiti za maoni ya wapigakura, ambazo zinaonyesha kuwa chama chake kitakabiliwa na wakati mgumu katika uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba.

https://p.dw.com/p/40898
Deutschland | Nach Flutkatastrophe im Ahrtal | Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Kiongozi huyo atakayeondoka baada ya miaka 16 madarakani, amesema chama hicho, Christian Democratic Union (CDU) kilifahamu fika tangu mwanzo kuwa haitakuwa kazi mteremko kushinda uchaguzi baada ya uongozi wake wa muda mrefu.

Soma zaidi:Kansela Merkel amnadi mgombea ukansela Armin Laschet

Matoleo ya hivi karibuni ya ripoti za utafiti wa maoni ya wapigakura nchini Ujerumani, yameonyesha kuwa Armin Laschet, mgombea wa chama cha CDU yuko katika nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa chama cha Social Demokratic, SPD huku umaarufu wake ukiwa umeshuka hadi asilimia 20.

Muda unayoyoma

Mbaya zaidi ni kwamba chama hicho cha Bi Merkel hakina muda wa kutosha kuweza kubadilisha mkondo wa mambo kabla ya uchaguzi wa bunge wa tarehe 26 Septemba.

DW Bundestagswahl 2021 Triell Baerbock Laschet Scholz
Wagombea wakuu katika uchaguzi mkuu wa Septemba nchini Ujerumani: (Kuanzia kushoto) Armin Laschet (CDU/CSU), Annalena Baerbock (Chama cha Kijani) na Olaf Scholz (SPD).

Kansela Merkel ambaye kwa kiasi kikubwa amejitenga mbali na shughuli za kampeni, amesema walijua mapema kuwa kama chama hakuna uhakika wa moja kwa moja kuwa watasalia madarakani.

''Tulikuwa na mdahalo katika bunge la shirikisho wiki hii. Kilicho muhimu ni kile kitakachofanyika siku ya uchaguzi na ndio sababu sitaki kuingilia wala kutabiri chochote sasa hivi,'' amesema Kansela Merkel.

Soma zaidi:Uchaguzi wa Ujerumani: Ni upi urathi wa sera ya kigeni ya Merkel?

Amesema wataendelea kupambana hadi dakika ya mwisho na kuongeza kuwa ''kila mtu ndani ya CDU na CSU alijuwa kuwa hatuna nafasi ya moja kwa moja kurejea madarakani bila mapambano, baada ya miaka 16.''

Merkel awaponda wapinzani kuhusu sera za mrengo wa kushoto 

Lakini licha ya kutojihusisha kwa karibu na kampeni ya mrethi wake, siku chache zilizopita Kansela Merkel alikejeli uwezekano wa serikali inayokuja kuwa yenye kuegemea mrengo wa kushoto.

Deutschland, Berlin | Markus Söder beim Wahlkampfauftakt der CDU / CSU
Markus Soeder, kiongozi wa chama cha SCU ambaye anasema muda unayoyoma kwao kuweza kupata ushindiPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Naye Markus Soeder, kiongozi wa chama cha Christian Social Union, SCU ambacho ni chama ndugu na CDU cha Kansela Merkel ametoa kauli inayodhihirisha kutambua mlima mrefu ambao unaukabili muungano wa vyama hivyo katika uchaguzi ujao.

Soeder ambaye pia ni waziri kiongozi wa jimbo la Bavaria kusini mashariki mwa Ujerumani, amesema ikiwa bado wanayo nafasi ya kushinda, nafasi hiyo ni mwishoni mwa juma hili.

Soma zaidi:Je, kiongozi wa chama cha Kijani Annalena Baerbock anaweza kuwa kansela ajae wa Ujerumani?

Alikuwa akimaanisha mkutano mkuu wa chama chake utakaoanza kesho Ijumaa hadi Jumamosi, na mdahalo wa pili kati ya mitatu ya televisheni, itakayowashirikisha wagombea wakuu katika kinyang'anyiro cha kurithi mikoba ya Kansela Angela Merkel. Mdahalo huo utafanyika Jumapili. Katika mdahalo wa kwanza uliofanyika Agosti 29, Armin Laschet alishindwa kung'aa.

SPD katika nafasi nzuri

Chama cha SPD kimenufaika na kuboreka kwa umaarufu wa mgombea wake, Olaf Scholz ambaye ni waziri wa sasa wa fedha. Scholz anapigiwa upatu kushinda uchaguzi huo wa kwanza tangu mwaka 1949 kutomshirikisha mgombea aliyeko madarakani.

Mbali na Armin Laschet wa muungano wa kihafidhina wa vyama vya CDU/SCU na Olaf Scholz wa SPD, mgombea mwingine mwenye nafasi ya kufanya vyema ni Annalena Baerbock wa chama cha Kijani, ambaye kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni yuko katika nafasi ya tatu.

 

ape,rtre