Uchaguzi wa Ujerumani 2021: Kutana na wagombea wakuu wa vyama
Huenda vyama sita vikawakilishwa katika bunge la Ujerumani, Bundestag, baada ya uchaguzi wa Septemba 26. Kutana na wagombea wakuu wa vyama hivyo, ambao watahudumu kama wasemaje wa vyama hivyo wakati wa kampeni.
Annalena Baerbock (chama cha Kijani)
Akiwa na umri wa miaka 40, Annalena Baerbock amekuwa mwenyekiti mwenza wa chama cha Kijani tangu mwaka 2018. Ni mwanasheria mwenye shahada ya sheria ya kimataifa kutoka Chuo cha Kiuchumi cha London, wafuasi wake wanamuona kama mtu anayestahili aliye na uelewa wa mambo. Wapinzani wake wanasema hana uzoefu wa uongozi.
Armin Laschet (CDU)
Armin Laschet ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Christian Democratic Union (CDU) na waziri mkuu wa jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu UJerumani. Wahafidhina walimpuuza Laschet mwenye umri wa miaka 60 ambaye anafahamika kwa imani yake ya utangamano na maridhiano. Lakini hivi majuzi imani hiyo imempelekea kujichanganya katika kauli zake kipindi hiki cha janga la virusi vya corona.
Olaf Scholz (SPD)
Huku kikiwa kinadidimia katika kila uchaguzi, chama cha Social Democratic SPD kimeamua kumchagua mwanahalisi badala ya mtu mwenye misimamo mikali kama mgombea wao. Waziri wa fedha Olaf Scholz, ambaye ni meya wa zamani wa Hamburg na makamu wa Kansela Merkel katika serikali kuu ya muungano na mwenye miaka 62 aliwashangaza wengi kwa umaarufu kwenye kura za maoni.
Christian Lindner (FDP)
Christian Lindner mwenye miaka 42 alijiunga na chama cha Free Democrats FDP akiwa na umri wa miaka 16 na amekuwa kiongozi wa chama hicho tangu mwaka 2013. Afisa huyu wa akiba na mtoto wa mwalimu anatokea jimbo la North Rhine-Westphalia na alisomea sayansi ya kisiasa. Anatazamia kujiunga na chama tawala baada ya uchaguzi wa Septemba na anataka kuwa katika serikali moja na vyama vya CDU/CSU.
Janine Wissler and Dietmar Bartsch (Left)
Dietmar Bartsch mwenye umri wa miaka 63 na Janine Wissler mwenye miaka 40 wanafaana. Bartsch anatokea Ujerumani mashariki na amekiongoza chama chake tangu 2015. Wisseler ambaye anaegemea siasa za mrengo wa kushoto anatokea Ujerumani magharibi na ameongoza chama hicho tangu Februari. Anawakilisha misimamo mikali ya chama chake kama kusitishwa kwa mipango yote ya kijeshi ya Ujerumani nje ya nchi.
Alice Weidel and Tino Chrupalla (AfD)
Tino Chrupalla mwenyekiti mwenza wa chama cha AfD alijiunga na chama hicho 2015 akivutiwa na sera yake ya kutopendelea wahamiaji. Chrupalla, mpakaji rangi kutoka jimbo la Saxony anakiunga mkono chama hicho cha mrengo wa kulia ila anasisitiza kutumika kwa lugha isiyo kali wakati wa kampeni. Alice Wiedel mwenye miaka 42 ni kiongozi mwenza wa AfD bungeni na mmoja wa viongozi maarufu wa chama hicho.
Wanasiasa hawa watakuwa wasemaje wakuu wa vyama vyao kipindi cha kampeni na watakuwa na jukumu muhimu katika siku za baadae. Iwapo vyama vyao vitaingia serikalini, basi watakuwa na uhakika wa kushikilia nyadhfa za uwaziri.