Uchaguzi wa rais wafanyika Syria
3 Juni 2014Rais Bashar al-Assad amepiga kura mjini Damascus, katika kituo cha kupigia kura cha Maliki hii leo asubuhi, katika uchaguzi ulio na wagombea wawili ambao hawana umaarufu sana nchini Syria.
Televisheni ya kitaifa nchini humo ilionyesha picha za Assad na mkewe Asma wakijitayarisha kupiga kura baada ya kujaza makaratasi ya kura ndani ya kijiofisi kilichokuwa karibu.
Picha nyengine zilizooneshwa katika vituo vya kupigia vilivyofunguliwa mapema leo ni maelfu ya watu waliopanga laini ndefu tayari kwa kupiga kura huku wengine wakioneshwa wakipeperusha bendera ya Syria ishara ya kumuunga mkono Assad aliye na umri wa miaka 48.
"Tunaomba kuwepo na usalama pamoja na udhabiti wa nchi," alisema Hussam al-Din mwalimu wa somo la kiarabu aliyekuwa wa kwanza kupiga kura katika kituo kimoja mjini Damascus.
Alipoulizwa nani atashinda alisema kwa sauti kwamba, kwa uwezo wa mwenyezi mungu Bashar Al Assad.
Kando na wale waliomsifu Assad na kumuunga mkono kuna na waleo walioona uchaguzi huu ni njia moja ya kupoteza wakati.
"Iwapo watu wetu waliokufa watarudi tena katika uhai, tupate viungo vyetu tulivyopoteza, nyumba zetu zilizoharibika, watu walioachwa bila makaazi kurejea katika makaazi yao, na iwapo Assad ataachia madaraka, basi tunaweza kuzungumzia uchaguzi lakini kwa sasa sio na Assad." Alisema raia mmoja wa Syria mjini Damascus.
Uchaguzi unafanyika katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali
Wapinzani wa Assad, wagombea wengine wawili wa kiti hicho cha rais nchini Syria, Maher al-Hajjar na Hassan al-Nuri wote walipiga kura zao mapema hii leo katika hoteli ya Sheraton.
Hata hivyo uchaguzi unafanyika tu katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali huku wapinzani walioko nje ya nchi wakiuita uchaguzi huo kama uchaguzi wa damu na Marekani nayo ikitoa tamko lake na kuuita uchaguzi huo kama muigo wa demokrasia.
Waasi nchini humo, wanasiasa wa upinzani walioko uhamishoni, mataifa ya Magharibi pamoja na mataifa ya Guba wote wanasema hakuna kura ya kuaminika inaweza kufanyika mahali ambapo mamilioni ya watu wameachwa bila makao kutokana na ghasia zilizoanzia na maandamano ya kutaka mageuzi hadi katika kuupinga utawala wa Assad.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ufaransa, France 2, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amesema uchaguzi huo ni masikitiko makubwa kuwa watu wanaokalia maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Syria wanamchagua Assad mtu aliyelelezewa na Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama mhalifu.
Kwa upande mwengine waasi wanaopigana na utawala wa Assad wameongeza mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ili kujaribu kuuvuruga uchaguzi.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef