Uchaguzi wa Rais Burundi:Kanisa Katoliki labainisha hitilafu
27 Mei 2020Baraza la maaskofu wa Kanisa Katoliki limesema waangalizi wake waliowekwa kwenye vituo vya kupigia kura nchini kote waliweza kushuhudia jinsi visanduku vya kura vilivyofanyiwa mizengwe na jinsi maafisa wa serikali walivyowabughudhi na kuwatisha wapiga kura. Baraza hilo pia limeeleza kuwa majina ya wakimbizi na ya watu waliokufa yaliwekwa katika daftari la wapiga kura.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP mwenyekiti wa baraza hilo la maaskofu Joachim Ntahondereye alitoa tamko kusema kwamba kura zilihesabiwa kwa siri na kwamba watu ambao hawakuhusika na masuala ya uchaguzi wailingia na kutoka ndani ya chumba cha kuhesabia kura.
Askofu huyo amesikitishwa juu ya hitilafu kadhaa zilizojitokeza kuhusu uhuru na kutokuwapo uwazi katika mchakato wa upigaji kura. Pia ameeleza kwamba baadhi ya wagombea na wapiga kura hawakutendewa haki. Kutokana na mazingira hayo, mwenyekiti huyo wa baraza la maaskofu nchini Burundi ameuliza iwapo matokeo ya uchaguzi hayakuwa na kasoro.
Hata hiyvo tume ya uchaguzi ilimtangaza mgombea wa chama tawala bwana Evariste Ndayishimiye kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 68.72 ya kura wakati mpinzani wake kiongozi wa chama cha upinzani bwana Agathon Rwasa aliambulia asilimia 24.19 ya kura. Chama cha upinzani kimeyapinga matokeo hayo kwa madai kwamba udanganyifu ulifanyika na kinapanga kwenda mahakamani hii leo.
Baadhi ya madai yaliyotolewa na kanisa katoliki yameshabihiana na yale yaliyotolewa na chama cha upinzani cha CNL. Chama hicho kimedai kwamba maafisa wake walitimuliwa kutoka kwenye vituo vya kupigia kura katika siku ya uchaguzi.
Katika siku ya uchaguzi hawakuwapo waangalizi wa kimataifa kwa sababu hawakuruhusiwa kuingia nchini Burundi. Afisa mmoja wa kanisa ambaye hakutaka kutajwa amesema maombi ya kanisa ya kupeleka waangalizi wao kwenye kila kituo cha kupigia kura nchini kote yalikataliwa, lakini kanisa liliweza kuwapeleka waangalizi wake karibu 3000 kwenye manispaa zipatazo 119 kwenye uchaguzi ulioendelea bila ya kuzingatia athari za janga la corona.
Uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na serikali ya rais Pierre Nkurunziza ulitatizika baada ya kanisa hilo kuupinga muhula wake wa tatu mnamo mwaka 2015. Watu wapatao 1200 walikufa kutokana na ghasia zilizosababishwa na uamuzi wa rais Nkurunziza wa kuendelea kubakia madarakani. Watu wengine laki nne waliikimbia nchi.
Vyanzo: AFP/DPAE